Saturday, 1 June 2019

Serikali kuanzisha kituo cha kuatamia ubunifu na biashara Chuo Kikuu Mzumbe


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Joyce Ndalichako amesema Wizara yake iko tayari kusaidia kutafuta  rasilimali kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kuatamia Ubunifu na Biashara “Innovation and Business Incubation Centre “ cha Chuo Kikuu Mzumbe, ambacho kitatoa fursa kwa wanafunzi wanaosoma katika Chuo hicho na Vyuo vingine na vijana wengine wenye mawazo ya kiubunifu, ujasiriamali na biashara, kuyaboresha mawazo na shughuli zao za kiubunifu ili ziweze kuwa biashara kamili.

Waziri Ndalichako amesema hayo katika kilele cha kambi ya ujasiriamali ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyofanyika katika Kampasi yake Kuu Morogoro ambapo amepongeza hatua hiyo ya kuanzishwa kwa kambi hiyo ambayo ni mara ya tatu inafanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017, huku akisema utaratibu huo ni tafsiri sahihi na kwa vitendo ya agenda ya Kitaifa ya kujenga Uchumi wa Viwanda.

 “Nimefurahi sana leo kuona bidhaa na ubunifu wa hali ya juu hapa na kusikia kuwa Kambi hii imeendelea kuvutia watu wengi, wakiwemo wanafunzi, baadhi ya wafanyakazi na watu wengine kutoka jamii zinazotuzunguka, utaratibu huu utakuwa na faida ya muda mrefu kwa Chuo kwani wahitimu wenu watakuwa wameiva kinadharia na kivitendo, na wenye uwezo wa kujiajiri na kutengeneza ajira”.  alisema.

Ndalichako amevitaka vyuo vingine kuiga mfano huu ambao unatoa fursa ya kukitangaza Chuo ambapo watanzania wataweza kujionea namna ambavyo fani mnazofundisha kama Uongozi wa Biashara, Ujasirimali, Uchumi na Mipango, TEHAMA, na zingine zinavyotayarisha wahitimu ambao wana mawazo ya kibunifu na ujasiriamali na mtazamo wa kibiashara.

Ndalichako amewataka Chuo Kikuu Mzumbe kuhahakisha kupitia kituo hicho atamizi kinawezesha wabunifu wao kushiriki katika mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), kwa lengo la kuhamasisha ubunifu nchini yanayoratibiwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.


Akizungumza katika kilele hicho Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka amesema kambi hiyo inashirikisha wanafunzi wa Mzumbe na wengine, wahitimu wa Mzumbe ambao ni wajasiriamali. Ameongezea pia kuwa kupitia kambi hiyo wanafunzi wenye mawazo ya kibiashara pia hukutanishwa na wafanyabiashara walibobea na ili kupata uzoefu.  Kusiluka ameahidi kusimamia uanzishwaji wa haraka wa kituo atamizi kwani kitasaidia kukuza mawazo ya kibunifu kuwa biashara kubwa nchini zitakazo changia pato la Taifa.

Nae mzungumzaji Mkuu wa kambi ya Mwaka 2019. Ndugu Ahmed Lussasi ambae ni mhitimu wa Chuo kikuu Mzumbe  na Mwazilishi mwenza wa kampuni ya MAXOM AFRICA, kampuni inayofanya vizuri katika biashara, amesema anapongeza wazo la kituo atamizi na ameiomba Serikali kulipa kipaumbele , kwani biashara yao ilianza kwa kulelewa katika kituo atamizi na hatimae kukua.  Lusassi kama mmoja wa wahitimu amekitaka Chuo kuwa na mfumo mzuri wa kushirikisha wahitimu wake katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya Chuo hicho.

Katika kambi hiyo Ndalichako amezindua bidhaa mbalimbali zilizobuniwa na wanafunzi wabunifu na wajasiriamli katika chuo hicho, ikiwa ni pamoja na kitabu kilichoandikwa na mwanafunzi wa Chuo hicho. Kwa mwaka 2019 wanafunzi 48 wameandikisha mawazo yao ya kibunifu ili yaweze kuboreshwa.

No comments:

Post a Comment