Imeelezwa kuwa vijiti na pamba za kusafisha masikio zinasababisha kwa kiasi kikubwa magonjwa ya usikivu yanayopelekea kuwa kiziwi.

Hayo yamebainika leo wakati wataalamu wa afya ya masikio na usikivu kutoka taasisi ya Starkey Foundation for Ear and Healing Care walipomweleza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea mabanda ya utoaji wa huduma za masikio na usikivu kwa wananchi mbalimbali jijini Dodoma.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Ummy amewataka wananchi kulinda masikio yao kwa kufuata ushauri wa madaktari na kuacha tabia ya kutumia vifaa vinavyosababisha matatizo ya usikivu kama spika za masikioni na matumizi ya pamba za kutolea uchafu.

“Tatizo la usikivu ni kubwa katika nchi yetu, katika tafiti ndogo ndogo ambazo zimefanyika zinaonesha asilimia 3 ya wanafunzi ambao wako shuleni wana matatizo ya usikivu kwa kiwango fulani lakini pia takwimu zinaonesha kuwa kila watu 100 wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza, 24 kati yao wanakua na matatizo ya usikivu”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri ummy amesema tafiti zinaonesha pia waathirika wengine wenye matatizo ya usikivu ni wale wanaofanya kazi katika migodi na viwandani hasa viwanda vya nguo ambapo takwimu zinaonyesha asilimia 50 wanakua na matatizo hayo.

Waziri Ummy ameishukuru taasisi ya Starkey Foundation for Ear and Healing Care kwa kutoa huduma za masikio na usikivu nchini huku akisema Serikali imeweka mikakati ya kuimarisha miundombinu, kununua vifaa na kuongeza wataalamu wa huduma za masikio na usikivu, kutoka wataalamu bingwa 11 mwaka 2009 mpaka kufikia wataalamu 46 mwaka 2018.

Hata hivyo Waziri Ummy amesema toka kuanzishwa kwa huduma hizi nchini kumesaidia kuokoa kupunguza idadi ya watoto kupelekwa India, ambapo kila mwaka takribani watoto 13 walikua wanapelekwa India kupata matibabu na mtoto mmoja alikua anagharimu Tsh. Milioni 80 mpaka Milioni 100. Lakini kuanzishwa kwa huduma hizi katika Hospitali ya Muhimbili mwaka 2017, watoto takribani 26 wamepata huduma kwa gharama ya Tsh. Milioni 35 na kuokoa fedha za Serikali kwa zaidi ya asilimia 60.

Kwa upande wake muanzilishi wa taasisi ya Starkey Foundation for Ear and Healing Care Dkt. Bill Austin ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma na vifaa vya masikio na usikivu kwa wananchi ambapo ilianza kutoa huduma hizo Jijini Mwanza na kuendelea kutoa huduma Jijini Dodoma.

MWISHO
Share To:

Post A Comment: