Friday, 14 June 2019

NDALICHAKO : TUNAENDELEA KUBORESHA SEKTA YA ELIMU.


Na EZEKIEL NASHON, DODOMA.

WAZIRI wa Elimu  Sayansi  na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, amesema serikali kupitia wizara ya elimu inaendelea kuboresha miondombinu katika elimu, ili kuhakikisha inaboresha sekta ya elimu hapa nchini.

Ameyasema hayo leo Jijini Dodoma katika maadhimisho ya wiki ya elimu iliyoenda sambamba na kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho ya  kumaliza elimu ya Msingi na Sekondari hapa nchini tukio lililofanyika Shule ya sekondari ya wasichana Msalato.

Amesema serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha inatoa elimu bora, ikiwamo kukarabati shule kongwe pamoja na vyuo vya ngazi zote sambamba na kuweka usimamizi thabiti katika vyuo ambayo vinazalisha walimu ili kupata walimu bora.

“Sisi kama serikali tunafanya jitihada kubwa kuhakikisha elimu yetu inapanda, tunahakikisha shule zote kongwe tunazikarabati angalau ziendane na hadhi ili watoto wetu wanasoma katika mazingira mazuri tukiwa pia tunasimamia kikamilifu vyuo vyetu vizalishe walimu ambao watatufikisha tunapotaka” amesema.

Katika sekta ya elimu ya ufundi amesema serikali imetenga kiasi cha bilioni ishirini na mbili(22) kujenga chuo cha veta katika mkoa wa Kagera ili kuinua sekta ya elimu ya ufundi sambamba na kuvikarabati vyuo vya veta kote nchini pamoja na kujenga  vyuo vipya katika wilaya mbalimbali hapa nchini ili kuinua elimu  ya ufundi.

Katika elimu ya juu amesema serikali imeboresha vyuo vikuu vyote na imejenga maktaba kubwa chuo kikuu cha Dar es saalam, yenye uwezo  wa kubeba wanafunzi wengi kwa wakati mmoja, pia imetenga zaidi ya bilioni sita(6) kujenga hosteli  katika chuo kikuu cha Mzumbe itakayoondoa changamoto ya makazi kwa wanafunzi.

Amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kuacha uzembe,  kwani  serikali imekuwa ikifanya  jitihada kubwa katika kuboresha elimu, wao kama hawatafanya jitihada kusoma  itakuwa kazi bure.

“Niwaambie wanafunzi serikali hata ikijenga magorofa au kuleta vitabu lori zima kama hamjitumi kusoma basi ni kazi bure ninashoowaomba ni ninyi kujituma katika kusoma ili jitihada hizi za serikali ziweze kuzaa matunda” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi  wa idara ya elimu kutoka TAMISEMI, Odilia Mushi, amevitaka vitengo vyote ya  elimu kutoka TAMISEMI kuhakikisha wanaimarisha   malezi kwa watoto ili waweze kupata  matokeo mazuri.

Amesema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa  ufaulu hapa nchini unaongezeka na umekuwa ukipanda mwaka baada ya mwaka na kuwataka wasimamizi kuweka njia nzuri katika kuhakikisha ufaulu unaongezeka zaid.

Katika tuzo hizo zimetolewa kwa wanafunzi kumi (10) bora wa shule za msingi waliofanya vizuri mitihani yao ya darasa  la saba, katika ngazi hiyo wanafunzi hao wamepewa vyeti na fedha kiasi cha laki tano(500,000) kila mmoja.

Kwa upande  wa kidato cha nne wanafunzi kumi bora katika ngazi hiyo wametuzwa vyeti na fedha kiasi cha  milioni moja(1,000,000) kila mmoja, kwa ngazi ya kidato  cha sita waliwekwa katika makundi matatu na kuwa na idadi ya wanafunzi tisa(9) ambapo kila mmoja ametuzwa vyeti na fedha taslimu milioni moja na laki  tano(1,500,000).

Zawadi nyingine zimeenda kwa  shule kumi bora kwa kila ngazi na kutunukiwa vyeti kila shule, na shule zile zilizoongeza ufaulu kutoka ngazi moja kwenda nyingine kwa kila ngazi ikiwa ni shule za msingi na sekondari kidato cha nne na sita.

No comments:

Post a Comment