Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Joyce Ndalichako amewaasa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Iringa kutumia mfumo wa elimu kuandaa vijana ambao watakuwa na mtazamo chanya  na mawazo ya kimaendeleo  yanayolenga kuja na majawabu ya changamoto mbalimbali zinatojitokeza katika jamii, ametaka vijana wajengwe katika kuona fursa zaidi.

Amesema hayo katika siku ya maadhimisho ya Kitivo cha Sayansi na Elimu katika Chuo Kikuu cha Iringa ambapo alikuwa mgeni Rasmi katika siku hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka Mkoani Iringa. Ndalichako amewataka vijana wanaosoma katika Chuo hicho kusoma kwa bidii ili  elimu wanayo ipata iweze kuwasaidia wao binafsi na jamii zinazowazunguka.

“Serikali yenu sikivu inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na kuboresha elimu nchini, kwa hili tumpongeze rais wetu, na kama kauli mbiu ya hapa kazi inavyosema, Rais na sisi  tunachapa kazi  ninyi kazi yenu ni kusoma kwa bidii ili mkimaliza muweze kushiriki moja kwa moja katika kujenga uchumi katika taifa letu”

Ndalichako amesema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa elimu ya juu kupitia Tume ya Vyuo Vikuu kwa lengo la kuhakikisha Vyuo vinatoa wahitimu bora na wenye sifa na ujuzi kwa ajili ya kuajiriwa na vile vile wenye ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na amewataka uongozi wa chuo hicho kuhakikisha kasoro zilizotolewa na TCU katika baadhi ya programu zao ambazo zimesitishwa zinarekebishwa kwa haraka ili zipate ithibati.  Ametumia nafasi hiyo pia kuwataka Vyuo Vikuu nchini kufuata Kanuni, Sheria na taratibu za uendeshajI Vyuo wakati wote.

 Akiwa chuni hapo ameongezea kuwa Serikali inathamini mchango wa sekta binafsi katika kutoa elimu huku akitolea mfano uwekezaji uliofanywa katika Chuo hicho na Serikali kwa  kutoa mitambo na vifaa mbalimbali vya Tehama vinavyowezesha utumiaji wa mkongo wa Taifa.

Awali akitembelea kituo atamizi cha chuo hicho, amepongeza juhudi mbalimbali zilizofanyika katika kituo hicho kwa kulea mawazo ya kibunifu hadi kufikia kutayarisha bidhaa, kuanzishwa biashara na kutoa mafunzo ya ujasiriamali na masoko kwa wanachuo na jamii inayowazunguka. Aidha amewataka vijana waliobuni bidhaa kuhakikisha  wanafuata taratibu za kurasimisha bidhaa zao.

Waziri Ndalichako amefurahishwa na uwezo mkubwa waliouonesha wanafunzi wabunifu walio katika kituo hicho na kuwataka kuendelea na mawazo na mtazamo wa kijasiriamali ambapo amesema hayo ni matokeo halisi ya mafunzo yanayotolewa katika na chuo hicho katika shahada ya ujasiriamali na Masoko kwa vitendo yaani “Bachelor of Applied Marketing and Entrepreneurship”.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa kinachomilikiwa na Kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania Prof.  Ndelerio Urio, amesema mwaka huu chuo kina wanafunzi zaidi ya 3,215. Amemshukuru Waziri kwa kutembelea Chuo hicho na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kusaidia vyuo Binafsi. Prof Urio  ameahidi kuendelea kusimamia ubora katika utoaji elimu ili kuendelea kutoa wahitimu bora akisistiza kuwa wataendela kujitathmini kila wakati ili kuhakikisha wanakuwa na programu bunifu zinakidhi mahitaji ya soko.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: