NA WAJMW-DODOMA

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mashindano ya taifa ya afya na usafi wa mazingira yatakayoratibiwa nchi nzima.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa bunge jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema lengo la mashindano hayo ni kuinua hali ya afya na usafi wa mazingira katika ngazi ya kaya na taasisi ili kulinda na kuboresha afya ya jamii.

“Mashindano haya yalianza mwaka 1988 ambapo yamekuwa yakifanyika kila mwaka. Kupitia mashindano haya hali ya usafi wa mazingira imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na kusaidia kupunguza magonjwa ya kuhara kutoka zaidi ya wagonjwa 1,300,000 mwaka 2014 hadi chini ya wagonjwa 70,000 mwaka 2018”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema mashindano hayo yamesaidia ujenzi wa madampo ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Arusha, Kigoma na Mtwara. Pia ujenzi wa machinjio ya kisasa katika miji mbalimbali  umeweza kutekelezwa na mashindano.

Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa mashindano hayo kwa mwaka 2019 yatahusisha Halmashauri zote 184 ambapo Halmashauri zitakazoshinda ngazi ya mkoa zitashindanishwa kitaifa, pia vipengele viwili vimeongezwa katika mashindano ya mwaka huu.

“Ili kuongeza chachu katika mashindano haya, Wizara imeongeza vipengele viwili ambavyo ni ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa na Taasisi za kibenki. Katika Mkoa Benki itakayoshinda itashindanishwa na mikoa mingine ili kupata mshindi wa kitaifa”. Amesema Dkt. Ndugulile.

Mashindano hayo yataendeshwa na kamati ya taifa ya mashindano ya usafi wa mazingira inayojumuisha wajumbe kutoka wizara na taasisi mbalimbali na pia yatakua  na muundo wa makundi 12 ambapo kila kundi litatoa washindi watatu. Makundi hayo ni Halmashauri za majiji na manispaa, Halmashauri za Miji, Halmashauri za Wilaya, Kijiji bora kinachotekeleza kampeni ya usafi wa mazingira, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za binafsi, Hoteli, Shule za sekondari na msingi, Shule za serikali za sekondari za bweni, Shule za binafsi za sekondari za bweni, Ofisi za umma na Mabenki.

Dkt. Ndugulile amesema Wizara imepanga kutoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa makundi ambapo watapatiwa fedha taslimu, vyeti na vikombe. Mshindi wa juu atatokana na kundi la Halmashauri za wilaya na atapata zawadi ya Shilingi Milioni Hamsini.

Hata hivyo, Dkt. Ndugulile ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambayo imewezesha kaya zake zote kuwa na vyoo bora. Naibu Waziri amesema usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo bora unaweza kupunguza magonjwa ya kuambukiza kwa zaidi ya asilimia 80 na hivyo kuipunguzia serikali gharama za kununua madawa na kupambana na magonjwa ya milipuko.

MWISHO
Share To:

msumbanews

Post A Comment: