Friday, 17 May 2019

WAZIRI MKUU MAJALIWA AITAKA CRDB WATOE ELIMU KABLA YA KUTOA MIKOPO ILI BIASHARA ZISIFE

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC),  Mei  17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mei 17, 2019 amefungua  Semina ya  Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Kituo cha Mikutano cha 
 Pichani, Mheshimiwa Majaliwa akiongozana  na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Mkutano huo, kuingia kwenye ukumbi wa Simba kufungua Semina hiyo. Kutoka kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kicheere, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya  Benki ya CRDB, Ally Hussein Laay na wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Musa Nsekela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Mheshimiwa Majaliwa akiongozwa   na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Semina hiyo kuingia kwenye kukumbi wa Simba ili  kufungua Semina hiyo. Kutoka kulia ni Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kicheere, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Ally Hussein Laay na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Musa Nsekela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Mheshimiwa Majaliwa akiongozwa   na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Semina hiyo kuingia kwenye kukumbi wa Simba ili  kufungua Semina hiyo. Kutoka kulia ni Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kicheere, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Ally Hussein Laay na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Musa Nsekela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Musa Nsekela wakati aliopowasili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)   kufungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB,  Machi 17, 2019. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Ally Hussein Laay, wa tatu kushoto ni Balozi wa Denmark nchini, Einar Hebogard Jensen na wapili kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Rota Sanare. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na viongozi baada ya kufungua Semina ya  Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Mei 17, 2019. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Ally Hussein Laay, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Musa Nsekela na wa tatu kushoto ni Balozi wa Denmark chini, Einar Hebogard Jensen.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Na Yusuph Mussa, Arusha


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Benki ya CRDB kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutoa mikopo, kwani baadhi ya waliopata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha wamejikuta wakishindwa kuendesha biashara zao ili kurejesha mkopo huo, na matokeo yake wananyang'anywa mali zao.


Aliyasema hayo leo Machi 17, 2019 wakati anafungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano jijini Arusha (AICC), Ukumbi wa Simba.


"CRDB mnatakiwa kutoa mikopo huku mkieleza matumizi bora ya fedha hizo za mkopo. Wananchi wengi wanaochukua mkopo huo, hawana elimu ya jinsi ya kutumia fedha hizo waweze kupata tija kwenye biashara au shughuli zao. Matokeo yake wanalia kwa kuchukuliwa nyumba zao, mashamba yao, magari yao, ng'ombe zao na mbuzi zao. Hivyo ni matumaini ya Serikali, mtaanza kutoa elimu kabla ya kutoa mikopo" alisema Majaliwa.


Majaliwa alisema moja ya mambo yanafanya taasisi za fedha zinakufa, ni kukosa usimamizi mzuri kutoka kwa menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi. Hivyo ameitaka Benki ya CRDB kuhakikisha inaboresha utendaji na uwajibikaji.


"Baadhi ya mashirika yamefilisika kutokana na kukosa utendaji na uwajibikaji. Na mwaka jana tumefunga benki tano kutokana na kukosa uwajibikaji, utendaji na Utawala Bora. Mtu yupo pale anataka kuchomoa fedha. Na hiyo ni kutokana na shughuli zetu kutoratibiwa vizuri. Hatutarajii hilo kutokea kwenye benki hii" alisema Majaliwa.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo alisema kutokana na Jiji la Arusha kuwa la kitalii, Benki ya CRDB iangalie uwezekano wa kuongeza muda wa kufanyakazi, ikibidi hata saa nne usiku angalau hata kwa tawi moja.


"Pia nashauri, kwa vile sasa hivi wajasiriamali wapo wengi, basi CRDB iangalie namna ya kuwainua wafanyabiashara hawa wadogo kwa kuwawezesha mikopo, ili watoke hapo kwenye umachinga na kuwa wafanyabiashara wakubwa kama Dkt. Reginald Mengi" alisema Gambo.


Gambo alisema utalii wa ndani bado muamko wake ni mdogo, hivyo Benki ya CRDB iangalie uwezekano wa kutangaza utalii wa nchi yetu kwa kuwapeleka wanahisa kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kila baada ama kabla ya kufanya Mkutano Mkuu wa mwaka.


Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Ali Laay alisema huu ni wakati wa wananchi kuchukua hisa, kwani baadhi ya watu wamewekeza kununua, nyumba, magari, mbuzi na ng'ombe, lakini uwekezaji mkubwa na endelevu ni wa kununua hisa, kwani hivyo vingine unaweza kufilisika, lakini wa kununua hisa kila siku utajiweza kimaisha.


Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema wamejipanga kuweza kuendesha benki hiyo kwa weledi ili wanahisa waweze kupata faida na kuona umuhimu wa wao kuwa sehemu ya benki hiyo. Pia kujenga uchumi wa nchi, uboreshaji huduma kwa wateja, kuongeza matumizi ya kifedha, huku wakiwa na matawi 263 nchi nzima.


"Lakini pia tunataka kuongeza ufanisi wa kibiashara, kuboresha mahusiano na Serikali na wadau wengine. Nia ikiwa kujenga uchumi wa nchi na uboreshaji huduma kwa wateja. Nia ni kuifanya benki ya kimkakati" alisema Nsekela.


Akichangia baadhi ya mada zilizotolewa kwenye semina hiyo, mmoja wa wanahisa Kapteni Mstaafu Noel Nkoswe kutoka Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, alisema kwa sasa hali ya uchumi kwa wananchi mmoja mmoja imeshuka, kwani wao kama wakulima  wa mahindi wameshindwa kupata soko, na sasa wamehamia kulima alizeti, lakini bado changamoto za kuuza zipo pale pale.


"Lazima tuzungumzie kushuka kwa uchumi kwa wananchi wetu, na hata kama Waziri Mkuu angekuwa bado yupo ukumbini ningemueleza. Hali  ni mbaya kwa wananchi. Wanalima mahindi, lakini bei ni ndogo. Biadhara za wananchi zinakufa, sio kwa sisi tuliopo vijijini tu, bali hata jijini Dar es Salaam maduka yamefungwa, kwani tunaona kwenye vyombo vya habari.


"Nawaomba wenzangu tuache kusifia kila kitu, ni lazima tukae na kujadili uchumi wa nchi yetu kuona ni namna gani tutajikwamua kutoka hapa tulipo. Mnanishawishi ninunue trekta la sh. milioni 68 kwa mkopo, lakini sitaweza kurudisha fedha hizo za mkopo, bali itabidi nikulipe mahindi ama alizeti, lakini sio fedha, maana sitapata fedha hizo" alisema Nkoswe.


MWISHO.


No comments:

Post a Comment