Saturday, 18 May 2019

Wabunge waunda kamati ya mashindano ya Walemavu Afrika MasharikiWabunge watano wa Bunge la Tanzania wameunda Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa watu wenye Ulemavu Afrika Mashariki (CECAAF) yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Mashindano hayo yashirikisha nchi tano wanachama ambazo ni wenyeji Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya na Rwanda.

Wabunge waliounda kamati hiyo ni William Ngeleja, Venance Mwamoto, Margret Sitta, Riziki Lulinda na Amina Mollel lengo likiwa ni kuhamasisha umma wa Watanzania kuyaunga mkono kwa hali na mali.

“Wizara yenye dhamana na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu inawaomba wananchi kuipa kamati hii ya wabunge ushirikiano wa kutosha katika maandalizi ya michuano hiyo ambayo yanahitaji fedha za kutosha na vifaa”, imeeleza sehemu ya taarifa iliyotolea leo na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe.

Mashindano hayo ambayo yatakuwa ya kwanza kufanyika katika ukanda huo, yameanzishwa kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Walemavu wa Mwaka 2006, unaotaka haki ya watu wenye ulemavu kushiriki katika mambo kadhaa ikiwemo michezo, izingatiwe.

No comments:

Post a Comment