Baadhi ya
washiriki kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake na vijana wenye nia ya
kutaka kugombea nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa
wilaya za Korogwe, Muheza, Handeni na Lushoto, ambapo mafunzo hayo
yaliyofanyika Mei 14 na 15, 2019, yameratibiwa na Taasisi ya Tanzania Youth
Coalition (TYC) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), na kufanyika mjini
Korogwe. Kulia ni mkufunzi Dkt. Ali Fungo.
Baadhi ya washiriki kwenye mafunzo
ya kuwajengea uwezo wanawake na vijana wenye nia ya kutaka kugombea nafasi
mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa wilaya za Korogwe, Muheza,
Handeni na Lushoto, ambapo mafunzo hayo yaliyofanyika Mei 14 na 15, 2019,
yameratibiwa na Taasisi ya Tanzania Youth Coalition (TYC) kwa ufadhili wa Umoja
wa Ulaya (EU), na kufanyika mjini Korogwe.
BAADHI ya viongozi wa vyama vya
siasa wanadaiwa kuchangia kukosekana kwa wagombea wanaokubalika kwa wananchi,
kwani kutokana na sheria kuwa huwezi kugombea bila kupitia kwenye chama,
kiongozi wa chama anatumia mbinu kuhakikisha hupati nafasi hata kama umeshinda
kura za maoni.
Hayo yamesemwa (Mei 14) kwenye
mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake na vijana wenye nia ya kutaka kugombea
nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa wilaya za Korogwe,
Muheza, Handeni na Lushoto, ambapo mafunzo hayo yameratibiwa na Taasisi ya
Tanzania Youth Coalition (TYC) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), na
kufanyika mjini Korogwe.
"Baadhi ya viongozi wa kisiasa
kwenye ngazi ya vijiji, kata na wilaya, wanachagua wagombea kwa maslahi yao.
Kiongozi anakufuata na kukuuliza vipi upo tayari nikusaidie kupita?
unaposhindwa kutimiza matakwa yake, anakuwekea alama za chini wakati wa majina
yenu kwenda kuchujwa ngazi za juu, matokeo yake jina lako linakatwa, hata kama
wananchi wanakupenda" alisema Majuto Mafiga kutoka kata ya Segera wilayani
Handeni.
Naye Upendo Kiangi kutoka Kata ya
Mazinde wilayani Korogwe alisema baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali
wanatumia nafasi ya ukoo mkubwa ama uzawa, hivyo ukiwa mgeni, yaani kutoka mkoa
mwingine huwezi kupata uongozi.
"Mimi nataka kugombea uongozi
kwenye kijiji ama kata yangu ya Mazinde, lakini nashindwa kupata kwa vile kuna
mgombea ukoo wake ni mkubwa. Yaani ukoo wake peke yake unatosha kumchagua kuwa
kiongozi. Sasa hiyo inakosesha nafasi kwa wengine, hasa ukiwa wa kuja (kutoka
mkoa mwingine)" alisema Kiangi.
Twalib Shafii kutoka Kata ya
Masuguru, Wilaya ya Muheza alisema angalau wana imani na utawala wa Awamu ya
Tano, vitendo vya rushwa vitapungua sana, kwani kwenye chaguzi zilizopita,
baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali walipita kwa rushwa, hivyo anaamini
vyombo vya dola vitakuwa makini kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na
Uchaguzi Mkuu mwakani.
Mkufunzi Dkt. Ali Fungo alisema
wakati wa uchaguzi ni lazima mgombea aheshimu maadili ya chama chake. Pia
anatakiwa kutoa ahadi zenye uhalisia na mahitaji ya wenyeji wa eneo husika.
"Huwezi kufanya kampeni kata ya
Mashewa (Korogwe) halafu ukaahidi kuwajengea kiwanda, wakati wao ni wakulima,
na wanahitaji zana za kilimo ili kufikia mahitaji yao" alisema Dkt. Fungo.
Mratibu wa Mradi wa Kuwawezesha
Wanawake na Vijana (WYPRE) katika Mkoa wa Tanga, ambao upo chini ya TYC Yahaya
Kitogo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa wanawake na vijana kugombea nafasi
mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
MWISHO.
Post A Comment: