Mkurugenzi wa Taasisi ya Progress Centre Rose Urio akizungumza kwenye uzinduzi wa zao la muhogo kitaifa lililofanyika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Mei 25, 2019, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo Omar Mgumba (Picha na Yusuph Mussa).
 Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela akizungumza kwenye uzinduzi wa zao la muhogo kitaifa lililofanyika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Mei 25, 2019, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo Omar Mgumba (Picha na Yusuph Mussa).
Naibu Waziri wa Kilimo Omar Mgumba (wa pili kulia) akiangalia muhogo uliokaushwa kutoka kwa mkulima Rajab Mzimu (kushoto) kutoka Kijiji cha Mabalanga wilayani Kilindi kwenye uzinduzi wa zao la muhogo kitaifa lililofanyika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Mei 25, 2019, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mgumba. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela. (Picha na Yusuph Mussa).
Na Yusuph Mussa, Kilindi


TAASISI ya Progress Centre imewahakikishia wakulima, Serikali na wadau wengine kuwa zao la muhogo halitakuwa tena kwa ajili ya kujikinga na njaa, bali kuwa la kiuchumi kwa kuongeza mapato kwa mkulima mmoja mmoja, huku Serikali ikilitegemea kuongeza pato la Taifa.


Ni kutokana na zao hilo malighafi yake kutumika kwenye viwanda zaidi ya 60 duniani kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali. Lakini pia kwa hapa nchini, baadhi ya viwanda vya bia vimeanza kutumia unga wa muhogo kutengeneza bia, hivyo ukiacha soko la nje, hata la ndani bado ni kubwa.


Hayo yalisemwa Mei 25 na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Rose Urio kwenye uzinduzi wa zao la muhogo kitaifa lililofanyika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo Omar Mgumba, huku Wilaya ya Kilindi ikichangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha uzinduzi huo, na tayari ikiwa imewaandaa vilivyo wakulima wake kulima zao la muhogo.


Urio ambaye anatumia kauli mbiu ya Cassava For Life (C4L) kuhamasisha zao la muhogo nchini, alisema mahitaji ya muhogo ni makubwa sokoni, kwani kuna viwanda tisa vya nguo nchini vinatumia wanga, na nyingi wanaagiza nje ya nchi. Pia kuna viwanda vya makaratasi zaidi ya vinne nchini vinavyotumia wanga katika uzalishaji wa karatasi, ambazo tunatumia kila siku.


"Mgeni rasmi, kampeni hii inayozinduliwa  leo tunategemea  italeta matokeo yafuatayo; mabadiliko ya mtazamo kuhusu muhogo kwamba sio zao la njaa na umasikini, na ni bidhaa yenye thamani kubwa. Kupunguza umasikini, kutengeneza ajira, idadi kubwa ya  Watanzania kushiriki katika ujenzi wa Taifa, kuongeza vyanzo vipya vya ulipaji kodi, na kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya Viwanda inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.


"Pia naomba nieleze kidogo, Cassava Flour (Unga wa Muhogo), viwanda vya bia vimeanzisha  bia itakayotengenezwa na unga wa muhogo. Tuna viwanda tisa vinavyotumia wanga kwa malighafi, na nyingi inaagizwa kutoka nje. Tuna viwanda vya makaratasi zaidi ya vinne vinavyotumia wanga katika uzalishaji wa karatasi tunazotumia kila siku, na mahitaji ya vyakula vya mifugo ni makubwa sana. Hizo ni baadhi tu ya bidhaa zitokanazo na mihogo.


Urio alisema uwepo wa Soko la China ni fursa kubwa. Kampeni itahimiza uratibu ulio makini ili kuhakikisha wakulima wanafikia soko hili, na wanunuzi wanapata bidhaa ambayo ni muhogo. Pia watahimiza ufafanuzi wa mkataba walioingia na China ili wafanyabiashara watakaopenda kwenda huko wauelewe vema.


Urio alisema ili kujua na kuona thamani ya jambo hilo, pia watahimiza matumizi ya kilimo cha mkataba, umuhimu wa kutunza fedha kwa kuweka akiba, kila mkulima ama kikundi kuwa na kalenda ya kilimo kwa kila msimu, kujiunga na mifuko ya jamii kama NSSF ili kupata huduma mbalimbali, umuhimu wa Bima ya Afya, umuhimu wa kuwa na bima ya mazao.


Mgumba alisema Taasisi ya Progress Centre limefanya jambo zuri kuweza kuwahamasisha wakulima kuchangamkia zao la muhogo, na wao Serikali wataweka mazingira mazuri kuona wakulima wanaondolewa mlolongo wa kodi, ushuru na tozo hasa kwenye pembejeo ili kilimo cha zao hilo kiweze kuleta tija na waweze kupata faida, kwani ili waweze kupata faida nzuri kwa zao hilo, wanatakiwa kulima zao hilo kwa kiwango kikubwa.


Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela alisema Serikali imetumia sh. milioni 200 kwa ajili ya kuwanunulia mbegu za muhogo wakulima, ambapo kati ya fedha hizo, Shirika la World Vision limetoa sh. milioni 60. Na katika kuondokana na kilimo cha jembe la mkono, Serikali, kupitia Shirika la Maendeleo (NDC), wamewakopesha wakulima wa mkoa wa Tanga matrekta 15, na kati ya hayo, 13 yamekopeshwa wilayani Kilindi.


MWISHO.
Share To:

Post A Comment: