Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 Bungeni Jijini Dodoma, leo tarehe 17 Mei 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 Bungeni Jijini Dodoma, leo tarehe 17 Mei 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 Bungeni Jijini Dodoma, leo tarehe 17 Mei 2019.

1.0             UTANGULIZI


1.  Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.  Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu lipitishe Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa Fedha 2019/2020.
2.   Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia siku ya leo tukiwa wazima wa afya njema na kuendelea kuijalia nchi yetu amani na mshikamano na kujadili bajeti hii inayolenga kusukuma mbele kasi ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo na wakulima kwa ujumla wao.
3.  Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniteua kuwa Waziri wa Kilimo. Pia, niwashukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayofanya kusukuma maendeleo ya nchi hii, ikiwemo Sekta ya Kilimo. Napenda kuwaahidi kwamba nitafanya kazi ya kuongoza Wizara ya Kilimo kwa uaminifu, juhudi na maarifa ili kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo zinawafikia walengwa ili kuongeza tija na kuinua kipato chao.
4.  Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa hotuba  yake ambayo iligusa maeneo mengi ikiwemo Sekta ya Kilimo. Aidha, nimpongeze tena Mhe. Waziri Mkuu kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kusimamia kilimo pamoja na maendeleo ya Vyama vya Ushirika.
5.  Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe na Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.) pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge kwa umahiri mkubwa.
 Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza Wabunge wote kwa umahiri wao mkubwa katika mijadala inayoendelea katika Bunge hili la Bajeti.
6.  Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji chini ya Uenyekiti wa Mhe. Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Dkt. Christine G. Ishengoma (Mb). Kamati ilipata fursa ya kukutana na Wizara na kutembelea baadhi ya maeneo kuona utekelezaji wa kazi za kilimo na kushauri namna ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara, Bodi na Taasisi zake. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, ushauri wao umezingatiwa na tutaendelea kushirikiana na Kamati ili kuleta mageuzi ya kilimo nchini.

2.0             MWELEKEO WA SEKTA YA KILIMO

7.  Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kubadilisha kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha, Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo umesisitizia mapinduzi ya viwanda na umeitambua Sekta ya Kilimo kuwa mhimili imara kwa ajili ya upatikanaji wa malighafi za viwanda.  Miongozo hiyo ya Kitaifa, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013, inatekelezwa na Wizara kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa kuongeza mitaji, teknolojia na ubunifu, Sekta Binafsi inashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa ASDP II.
8.  Mheshimiwa Spika, ASDP II iliyozinduliwa rasmi tarehe 4 Juni, 2018 na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inalenga kubadilisha maisha ya mkulima kwa kufanya mageuzi makubwa kwenye kilimo kwa kuzingatia mazao ya kipaumbele kulingana na ikolojia za kilimo. 

3.0             MCHANGO WA KILIMO KATIKA UCHUMI

9.  Mheshimiwa Spika, kilimo ni sekta kubwa na muhimu kwa maendeleo kutokana na mchango wake katika uchumi. Katika mwaka 2017, sekta hiyo imetoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia takriban asilimia 28.7 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao ilichangia asilimia 16.58.  Vilevile, Sekta ya Kilimo inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018, ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia asilimia 7.1. Ukuaji huo ulichangiwa na jitihada za Serikali za kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya  pembejeo bora, hali nzuri ya mvua na uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji.

3.1  Upatikanaji wa Chakula

10. Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa  chakula kwa mwaka 2018/2019 ulifikia tani milioni 16.89 zikiwemo tani milioni 9.53 za mazao ya nafaka na tani milioni 7.35 za mazao yasiyo nafaka. Kiwango hicho cha uzalishaji kimeiwezesha nchi kujitosheleza kwa mahitaji yake ya chakula ya tani milioni 13.56 na hivyo kuwa na ziada ya tani milioni 3.32 za chakula kwa kiwango cha utoshelevu cha asilimia 124. Niwahakikishie watanzania kwamba, tunacho chakula cha kutosha nchini.  Hata hivyo, tuendelee kuweka akiba katika kaya zetu hadi tutakapovuna tena kwani inaonekana kwamba huenda tusiwe na mavuno mazuri sana msimu huu kutokana na uhaba wa mvua kwenye maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kati na Kaskazini mwa nchi yetu.(Maelezo ya kina yanapatikana uk.5 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti).

3.2   Umwagiliaji

11. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia Mipango Shirikishi ya Maendeleo ya Rasilimali za Maji. Katika mpango huo, hekta 560,880 zimepangwa kuendelezwa kwa lengo la kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 475,052 mwaka 2018/2019 hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2035. (Maelezo ya kina yanapatikana uk.6 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti)

3.3   Maendeleo ya Ushirika

12. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika kwa kusimamia na kuhamasisha maendeleo yake. Vyama vya Ushirika vimeongezeka kutoka vyama 10,990 Desemba 2017 hadi vyama 11,331 kufikia Desemba 2018. Vilevile, idadi ya wanachama wa vyama vya ushirika imeongezeka kutoka 2,619,311 mwaka 2017 hadi 3,998,193 Februari, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 53.
Hadi Desemba 2018, mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.3 imetolewa kwa wanachama ikilinganishwa na Shilingi bilioni 902 iliyotolewa kufikia Desemba 2017.

 Aidha, Akiba na Amana za wanachama katika SACCOS zimefikia Shilingi bilioni 575 na hisa Shilingi bilioni 79. (Maelezo ya kina yanapatikana uk.7 wa kitabu cha Hotuba ya bajeti)

4.0             UTEKELEZAJI WA MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2018/2019

13. Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2018/2019, Wizara imetekeleza  maeneo ya kipaumbele ya kuongeza tija kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia kwa mazao ya mahindi, muhogo, ngano, michikichi, ufuta, alizeti, pamba na mpunga.
14.  Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ya kipaumbele ni kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora za mazao na kusambaza kwa wakulima; kuboresha maarifa na ujuzi kwa watafiti; kuimarisha huduma za upimaji wa matabaka na ubora wa udongo kuendana na mahitaji ya mazao ya kilimo ki-ikolojia; mafunzo na usambazaji taarifa za kilimo na sayansi shirikishi; kusajili na kuandaa kanzidata ya wakulima na kuimarisha ushirika. (masuala yote ya utekelezaji wa maeneo ya kipaubele yapo kwa kina kwenye ukurasa 10-61  katika kitabu cha Hotuba ya bajeti)
15. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza vipaumbele hivyo, Shilingi bilioni 204.07 ziliidhinishwa na Bunge lako Tukufu. Kati ya fedha hizo, Fungu 43 – Wizara ya Kilimo iliidhinishiwa Shilingi bilioni 166.26zikiwemo Shilingi bilioni 68.14 za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 98.12 za matumizi ya maendeleo; Tume ya Taifa ya Umwagiliaji - Fungu 05 iliidhinishiwa Shilingi bilioni 29.77 zikiwemo Shilingi bilioni 3.95 za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 25.82fedha za maendeleo; na Tume ya Maendeleo ya Ushirika - Fungu 24 iliidhinishiwa Shilingi bilioni 8.05 zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida.

4.1  Kuongeza Tija katika Kilimo

Upatikanaji wa mbegu bora za mazao
16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019,  upatikanaji wa mbegu bora umefikia tani 49,040.66. Kati ya kiasi hicho, tani 38,507.87 zimezalishwa hapa nchini, tani 8,361.46 zimeagizwa toka nje ya nchi na tani 2,171.33 ni bakaa ya msimu wa 2017/2018. Vilevile, miche 1,507 ya miwa, vipando 121,805 vya muhogo na vikonyo 520,000 vya viazi lishe vimezalishwa. Aidha, aina mpya 13 za mbegu bora zimeidhinishwa na zitaanza kuzalishwa msimu wa 2019/2020.
Upatikanaji na udhibiti wa ubora wa Mbolea
17. Mheshimiwa Spika, hadi Machi 2019, upatikanaji na usambazaji wa mbolea nchini ulikuwa tani 492,394 ikilinganishwa na mahitaji ya tani 514,138 katika msimu wa 2018/2019. Aidha, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefanya ukaguzi kwa wauzaji wa mbolea 1,350 na wafanyabiashara 496 wapya wa mbolea  wamesajiliwa.

Upatikanaji wa Viuatilifu na Udhibiti wa Visumbufu
18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imenunua lita 296,000 na kilo 3,000 za viuatilifu vyenye thamani ya Shilingi bilioni tisa (9) kwa ajili ya kukabiliana na milipuko ya visumbufu vya mazao. Hadi kufikia Machi 2019, ndege waharibifu wa nafaka walidhibitiwa katika skimu za umwagiliaji za Kahe, Lekitatu na Misenyi kwa mazao ya mpunga na mtama.  Aidha, lita 119,000 kwa ajili ya kudhibiti Viwavijeshi Vamizi zimesambazwa katika Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Mashariki na kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima 350.

Zana za Kilimo
19. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kwamba wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya  matrekta na asilimia 24 ya wanyama kazi mwaka 2013. Kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua na kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa mwaka 2013.  Aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara imendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo. Katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, mikopo 33 yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.50imetolewa.

4.2  Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umwagiliaji

20.  Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Maendeleo ya Umwagiliaji imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mradi wa  Skimu za Umwagiliaji za Wakulima Wadogo unaofadhiliwa na Serikali ya Japan. Mradi umekarabati skimu za umwagiliaji 129 katika Halmashauri 68 nchini pamoja na ununuzi wa mitambo ya ujenzi. 

4.3   Utafiti wa Kilimo na Uhaulishaji wa Teknolojia

21.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia TARI imegundua mbegu bora mpya aina nne (4) za mahindi. Mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno kwa wastani wa tani 5.8 kwa hekta kwenye mashamba ya wakulima katika ukanda wa chini na kati, zinahimili ukame na zina ukinzani wa magonjwa ya majani ya mahindi na michirizi na ukungu. Vilevile, kwa kushirikiana na kampuni binafsi, TARI imezalisha aina sita (6) ya miche ya mbegu bora ya migomba na kugundua aina 62 za  mbegu za mazao ya mikunde.

4.4  Maendeleo ya Mazao

22.  Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya  mazao mbalimbali  kwa kuimarisha huduma za utafiti, upatikanaji na utumiaji wa pembejeo na zana za kilimo, udhibiti wa visumbufu vya mazao, huduma za ugani, uongezaji wa thamani na upatikanaji wa masoko. Aidha, Wizara imeandaa mkakati wa miaka minne (2018/2019 – 2021/2022) wa  kuendeleza zao la michikichi.
Mazao Makuu ya Asili ya Biashara
23.  Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao makuu ya biashara uliongezeka kutoka tani 901,641 msimu wa  2016/2017 hadi tani 967,184 msimu wa 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.2. Katika msimu wa 2018/2019, Wizara ililenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara hadi kufikia tani 1,356,368 na hadi kufikia Machi 2019, tani 667,631.77 sawa na asilimia 49.2 ya lengo zilikuwa zimezalishwa na uzalishaji unaendelea.
24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, uzalishaji wa mazao ya bustani ulikuwa tani milioni 5.33 na matarajio ya uzalishaji kwa mwaka 2018/2019 ni tani milioni 5.96. Hadi Machi 2019, uzalishaji umefikia tani milioni 4.36 sawa na asilimia 73.17 ya lengo na msimu wa uzalishaji unaendelea.

4.5  Ujenzi wa Miundombinu ya Kuhifadhi Mazao ya Kilimo na Masoko

Miundombinu ya Kuhifadhi Mazao ya Kilimo
25. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kutekeleza Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka. Hadi kufikia mwezi Machi 2019, asilimia 83 ya vifaa  vilikuwa vimeingizwa nchini kwa ajili ya ujenzi wa ghala katika vituo vya Makambako, Mbozi, Songea, Shinyanga na Dodoma.
Masoko ya Mazao ya Kilimo
26. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imeanzisha kitengo cha masoko ya mazao ya kilimo ambacho kinahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara imeingia makubaliano ya Itifaki ya Usafi baina ya Tanzania na Serikali ya China kuwezesha kuuza muhogo nchini China ambapo hadi mwezi Machi 2019, kampuni tano zimesajiliwa kwa ajili ya kuuza zao hilo nchini China.


Hifadhi na Usalama wa Chakula
27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, NFRA imenunua tani 46,236.035 za mahindi kwa ajili hifadhi na imeliuzia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani tani 36,000 za mahindi zenye thamani ya Shilingi bilioni 21.  Aidha, Wizara imeanza kutekeleza Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu katika mazao unaolenga kudhibiti tatizo la sumukuvu katika mazao ya mahindi na karanga.

4.6  Huduma za Ushauri Kuhusu Utafiti, Mafunzo na Usambazaji Taarifa za Kilimo na Sayansi Shirikishi

Huduma za Ugani
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imeandaa rasimu ya  Mwongozo wa Utoaji na usimamizi wa huduma za ugani utakaotumiwa na Sekta ya Umma na Binafsi. Aidha, elimu kuhusu kanuni bora za uzalishaji wa mazao, kuongeza thamani mazao ya kilimo, upatikanaji wa masoko, mitaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye kilimo, pembejeo na zana bora za kilimo imetolewa kupitia maonesho na vyombo vya habari.






Vyuo na Vituo vya Mafunzo ya Kilimo
29. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitia Vyuo vyake vya Kilimo  imedahili na kufundisha wanafunzi 2,389 ambapo wanafunzi 2,051 wamefadhiliwa na Serikali  na 338 wanajilipia wenyewe.  Kati ya  wanafunzi waliodahiliwa, wanafunzi 1,537 ni ngazi ya Astashahada na 852 ni  ngazi ya Stashahada. Jumla ya wanafunzi 1,026 wakiwemo 263 wa Stashahada na 763 wa Astashahada watahitimu masomo yao mwezi Juni, 2019.

4.7  Kuimarisha Ushirika

30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Tume ya Maendeleo ya Ushirika kupitia Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limefanya ukaguzi wa nje kwa vyama vya ushirika 2,297. Kati ya Vyama vilivyokaguliwa, asilimia 4.6 vilipata hati inayoridhisha, asilimia 64.6 vilipata hati yenye shaka, asilimia 21.6 vilipata hati isiyoridhisha na asilimia 9.2 vilipata hati mbaya. Hali hiyo ya Vyama vya Ushirika siyo nzuri na hatuwezi kuifumbia macho. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yetu tuendelee kushirikiana na Halmashauri zetu kuvisaidia vyama hivi ambavyo ni mkombozi wa mkulima.

4.8   Usajili wa Wakulima

31. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza usajili wakulima wote kwa mazao ambayo yanasimamiwa na Bodi.  Mazao hayo ni, kahawa, korosho, miwa, pamba, chai, mkonge, tumbaku na pareto. Hadi kufikia mwezi Machi 2019, wakulima 1,464,827 wametambuliwa na kusajiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

4.9  Masuala Mtambuka


32.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara imeendelea kuzingatia masuala mtambuka katika kutekeleza majukumu yake. Masuala hayo ni pamoja na ushiriki wa vijana katika kilimo, lishe, jinsia, hifadhi ya mazingira na VVU na UKIMWI.

5.0             MPANGO NA MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2019/2020

5.1  Kuongeza Tija katika Kilimo

    Upatikanaji wa mbegu bora za mazao
33.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, imejipanga kuzalisha jumla ya tani 53,608.2 za mbegu mbalimbali. Wazalishaji hao ni pamoja na ASA, Vituo vya Utafiti, Magereza na Sekta binafsi. Vilevile, ASA itazalisha vipando bora vya mihogo pingili 7,000,000 na miche bora ya matunda 20,000. Ili kufikia malengo hayo, miundombinu ya umwagiliaji itaboreshwa katika mashamba yanayomilikiwa na ASA na eneo la uzalishaji wa mbegu litaongezwa hadi kufikia hekta 811 katika mashamba mbalimbali.
Upatikanaji na udhibiti wa ubora wa Mbolea
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020, Wizara itasimamia uagizaji na usambazaji wa tani 625,000 za mbolea zinazokadiriwa kutumika nchini. Aidha, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) itaongeza mauzo ya mbolea kutoka tani 10,000 hadi tani 100,000. Vilevile, ghala moja (1) lenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 za mbolea litakarabatiwa katika wilaya ya Tabora pamoja na kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchanganya mbolea kwa uwiano (blending plant) katika Mkoa wa Dar es Salaam. 
Upatikanaji wa Viuatilifu na Udhibiti wa Visumbufu
35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020,

Share To:

msumbanews

Post A Comment: