Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) sambamba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakiimba wimbo wa mshikamano wakati akifungua  mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo tarehe 24 Mei 2019, wengine pichani ni viongozi wa TUGHE na RAAWU. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akitoa maelezo ya awali wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo tarehe 24 Mei 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua  mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo tarehe 24 Mei 2019, wengine pichani ni viongozi wa TUGHE na RAAWU.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakiwa katika picha ya pamoja na  wafanyakazi wa wizara ya Kilimo ambao ni wajumbe wa Baraza la wafanyakazi lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo tarehe 24 Mei 2019, wengine pichani ni viongozi wa TUGHE na RAAWU.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Awamu ya Tatu ya Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa (2017-2022 ina mtizamo mpya unaolenga kuhakikisha kuwa rushwa inaondolewa nchini kwa kutumia mbinu mpya na zinazotekelezeka kwa kuweka mkazo katika sekta zenye mazingira shawishi ya rushwa.

Utekelezaji wa Mkakati huo unalenga kupunguza na kudhibiti rushwa katika sekta/ maeneo muhimu ya kimkakati ambayo ni pamoja na manunuzi ya umma, ukusanyaji wa mapato, utoaji wa haki, maliasili na utalii, madini, nishati, mafuta na gesi, afya, elimu na ardhi.

Rushwa ni adui wa haki, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akifungua  mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa Mikutano uliopo katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) leo tarehe 24 Mei 2019 amekemea na kuwataka watumishi kupambana na rushwa katika sehemu za kazi.

Amewataka watumishi kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma kwa kutoshiriki katika kutoa au kupokea rushwa. “Napenda kusisitiza kuwa yeyote atakayejihusisha na kubainika kupokea au kutoa rushwa hatua stahiki na kali zitachukuliwa dhidi yake” Alikaririwa Mhe Hasunga

Waziri Hasunga amesema kuwa bado wizara inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake kutoa huduma kwa umma ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha na rasilimali watu wa kutosha, hali inayosababisha kutofikiwa kwa malengo. “Niwahakikishie kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto hizo. Ni matumaini yangu kuwa, mkiwa kama Wataalamu mtatumia uwezo wenu katika kuibua mikakati itayosaidia kuwezesha Kilimo kuwa chenye tija na cha kibiashara” Alisisitiza

Kadhalika, amewataka watumishi wote kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili katika Utumishi wa Umma.

Mhe Hasunga amesema kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kwa Mtumishi yoyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na vitendo vinavyokiuka maadili ya Utumishi wa Umma.

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli inayo dhamira ya dhati ya kuondoa uzembe na ubadhirifu miongoni mwa watumishi wa umma na hivyo mtumishi anaruhusiwa kudai haki zile za msingi kwa kuzingatia Kanuni, Sheria  na Taratibu za Utumishi wa umma wakati wa kutekeleza wajibu wake wa msingi kwa Mwajiri na kwa kutumia lugha ya staha.

Vilevile serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya Mwajiri na watumishi kwani pasipokuwa na ushirikiano wa pande hizo mbili, ni vigumu Taasisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Umuhimu huu wa mashirikiano, umetiliwa mkazo kupitia Sera, Sheria na Kanuni zinazosimamia uendeshaji Taasisi za Umma.

Amesema kuwa ili kuweza kutafsiri dhana hiyo, ni muhimu pia kwa pande zote mbili kutambua haki na wajibu katika utekelezaji wa majukumu ya kazi, kwani umekuwepo utamaduni wa baadhi ya watumishi kudai haki bila kutimiza wajibu wao kwa Mwajiri.

MWISHO

Share To:

Post A Comment: