Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto), akizungumza na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Geita, wataalamu kutoka wizarani, TANESCO na REA katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Aprili 20, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.

Na Veronica Simba – Chato

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amekutana na wakandarasi wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Geita na kujadiliana kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi zaidi.

Katika kikao hicho kilichofanyika leo, Aprili 20, 2019 katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chato, makubaliano maalum yaliyofikiwa ni kwa wakandarasi husika kuhakikisha wanakamilisha Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa kwanza, mkoani humo ifikapo Septemba mwaka huu.

Akiwapa hamasa ya kufanya kazi kwa viwango na kasi, Waziri Kalemani amewaambia wakandarasi hao kuwa siyo dhambi kukamilisha kazi waliyopewa kabla ya muda ulioanishwa katika Mkataba wao.

Aidha, amewataka kujenga utaratibu wa kuwashirikisha viongozi wa maeneo wanakotekeleza miradi husika wakiwemo Wakuu wa Wilaya, wabunge na madiwani ili pamoja na mambo mengine waweze kuwaelimisha wananchi na kufuatilia ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Wataalamu kutoka wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), pia wameshiriki kikao hicho.

Waziri wa Nishati yuko mkoani Geita kwa ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: