Na Thabit Hamidu, Zanzibar

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kufuatilia mienendo ya watoto wa kike ili wapate malezi bora yatakayowaepusha na changamoto za udhalilishwaji wa kijinsia.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) anayefanyia kazi zake Zanzibar. Tunu Juma Kondo katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa Kamati tekelezaji ya UWT Wilaya ya Dimani kichama.

Alisema wazazi,walezi na jamii kwa ujumla inatakiwa kuwa karibu na watoto wa kile ambao kwa sasa wanaishi katika mazingira hatarishi ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji vinavyopelekea kuwakosesha haki zao za msingi zikiwemo elimu,uongozi na haki ya kuishi huru.

Alisema wazazi wahakikishe watoto kila wanapotoka kwenda skuli na sehemu zingine za kijamii wakaguliwe mikoba yao kwani wengine wanaondoka na nguo za ziada na kwenda sehemu za starehe hali inayopelekea kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Alieleza kuwa jukumu la malezi ya watoto ni jukumu la kila mtu hivyo pindi watoto wakionekana katika mazingira hatari wananchi wa mtaa husika wanatakiwa kuchukua hatua za kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi ama kwa wazazi husika.

Alibainisha kwamba kuna baadhi ya wanaume wasiokuwa na maadili mazuri wamekuwa ni chanzo cha kuwadanganya na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji watoto wa kike hasa wanaosoma shule za maandalizi na msingi,jambo ambalo ni kinyume na mila,desturi na utamaduni wa kizanzibar.

Naibu Katibu Mkuu huyo Tunu, aliweka wazi kuwa CCM kupitia UWT Zanzibar itaendelea kulaani vitendo vyote visivyofaa vinavyokatisha malengo ya maendeleo ya wanawake nchini na kuishauri serikali ichukue hatua stahiki kwa wahalifu wote wa matukio ya udhalilishaji.

Akizungumzia uimarishaji wa CCM Tunu, aliwataka Wanawake hao kulipa ada za uanachama kwa wakati ili kurahisisha mipango ya kiutendaji ya Chama na Jumuiya kwa ujumla
Share To:

msumbanews

Post A Comment: