Thursday, 18 April 2019

Watoto wa kike wametakiwa kuchangamkia fursa ya Elimu


Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo amewataka watoto wa kike kuchangamkia fursa ya elimu ili kupata wasomi wanawake wenye sifa za kuwa viongozi wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Wito huo ameutoa katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa Kamati Tekelezaji ya UWT Wilaya ya Kaskazini ‘A’ huko Gamba Mkoa wa Kaskanizi Unguja, alisema elimu ndio nyenzo pekee ya kuwakomboa kiuchumi na maendeleo wanawake nchini.

Ameeleza kwamba kwa sasa watoto wa kike wanatakiwa kujengewa mazingira rafiki ya kupewa elimu bora itakayowasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Alisema wanawake wanaopewa fursa mbali mbali za uongozi,utendaji na utaalamu wa fani mbali mbali katika jamii wamekuwa mfano wa kuigwa katika utendaji na uchapakazi wao hivyo hicho ni kipimo sahihi cha uadilifu uliotukuka kwa kundi hilo.

Alisema kwamba mararajio ya UWT Zanzibar ni kuona wanawake wanajitokeza kwa wingi kushindana na wanaume katika kuwania nafasi mbali mbali za uongozi katika chaguzi mbali mbali za kisiasi zijazo kwani wanawake wengi wana sifa za kiutendaji.

Alisema kila mwanamke anatakiwa kuchukua hatua ya kuwalinda na kuwasimamia watoto wa kie dhidi ya vitendo vya udhalilishwaji ili waweze kutimiza malengo yao bila kukatishwa na baadhi ya watu wanaokwamisha juhudi za kundi hilo kijamii.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo ndugu Tunu, alisema anawashukru akina mama wote walioshiriki kumuombea dua na kumuunga mkono kwa kumuona anafaa kuongoza nafasi hiyo na hatimaye akateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo.

Alieleza kwamba atakuwa kiongozi na mtendaji mchapakazi anayetekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na kushauriana na watu anaowaongoza ili kufikia malengo mahsusi ya jumuiya hiyo.

Alisema ni lazima viongozi na watendaji wa Umoja huo wafanye kazi kwa bidii ili kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Ibara ya Tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo Jipya la mwaka 2017 inayoeleza namna CCM inavyotakiwa kushinda kwa kishindo kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Dola

No comments:

Post a Comment