Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi bora wa mwaka 2019 kwa kuwashindanisha wafanyakazi bora saba (7) kutoka Idara na Vitengo vya ofisi hiyo ambao wamepatikana kwa kigezo cha utendaji kazi mzuri kupitia Mfumo wa Wazi wa Mapitio ya Utendaji Kazi (OPRAS).
Mfanyakazi bora aliyechaguliwa ni Afisa Tawala, Jafari Kalaghe kutoka Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu.
Mara baada ya kumtangaza  Kalaghe kuwa mfanyakazi bora, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mick Kiliba, amempongeza kwa ushindi na kuwashukuru watumishi kwa kufanya uchaguzi uliozingatia vigezo.
Kiliba amesema kuwa, Kalaghe ni mchapakazi hodari anayeonekana na kila mtu na amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza kabla ya uchaguzi, Kiliba, aliwataka watumishi kumchagua mtumishi ambaye utendaji kazi wake unaonekana kuwa ni bora badala ya kuchagua kwasababu za kufahamiana.
“Tunapopiga kura, tusimchague mtumishi kwasababu unamfahamu au anatoka kwenye idara au kitengo kimoja, bali tumchague kwa uchapakazi wake unaoendana na kauli mbiu ya HAPA KAZI TU, inayohimizwa na Serikali ya Awamu ya Tano,” Kiliba ameongeza.
Kwa upande wake, mfanyakazi bora aliyechaguliwa, Jafari Kalaghe amewashukuru watumishi kwa kuona utendaji wake na kuahidi kuendelea kuchapa kazi kwa ushirikiano.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: