Saturday, 27 April 2019

UCSAF KUJA NA ZABUNI BILIONI 26

Na Furaha John,Dodoma.

MFUKO wa Mawasiliano kwa wote(UCSAF), umesema ifikapo Mei mwaka huu unatarajia kutangaza zabuni ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 214 zenye vijiji 521 itakayogharimu Sh.Bilioni 26.5.

Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, Mhandisi Peter Ulanga, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa kuhusu maadhimisho ya miaka 10 ya Mfuko huo yatakayozinduliwa April 27  na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Ulanga amesema kuwa ifikapo Mei mwaka huu watatangaza zabuni ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata na vijiji hivyo ambapo utekelezaji utaanza mara moja baada ya tathimini kukamilika mwishoni mwa juni mwaka huu.

Mtendaji mkuu huyo amesema bado kuna maeneo ambayo hayana huduma za mawasiliano ambapo mfuko huo umejikita kuhakikisha yanapata huduma muhimu na mwezi Mei mwaka huu mfuko utatangaza zabuni ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 214, zenye vijiji 521.

Pia amesema, serikali itatenga fedha kwa ajili ya maandalizi ya zabuni nyingine yenye vijiji zaidi ya 500 itakayotangazwa katika mwaka wa fedha 2019/20 kwa gharama ya Sh.Bilioni 26.
Mtendaji huyo akizungumza kuhusu  mafanikio ya mfuko,kiasi cha Sh.Bilioni 118 kimetumika kufikisha mawasiliano tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 ndani ya kipindi cha miaka 10.
Ulanga amesema, serikali kupitia mfuko huo imekwisha kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 703, zenye vijiji 2,501 na wakazi zaidi ya milioni tano kote nchini.
"Mchango huo wa serikali ni wastani wa asilimia 26 ya gharama za ujenzi na uendeshaji wakati watoa huduma wamechangia asilimia 74 kufanikisha uwekezaji huo," amesema.

Ametanabaisha kuwa tangu kuanzishwa kwa mfuko huo umejikita kutambua mahitaji ya mawasiliano nchi nzima, kushirikiana na wadau mbalimbali wa mawasiliano nchini, kushirikisha wananchi katika kutambua na kutatua kero za mawasiliano.

Amesema, wakati mfuko huu unaanza takribani asilimia 45 tu ya watanzania walikuwa wanaishi katika maeneo yaliyofikiwa na mawasiliano ya simu, mpaka tunavyoongea leo takribani asilimia 94 ya watanzania wanaishi kwenye maeneo yanayofikiwa na mawasiliano ya simu ambapo zaidi ya asilimia 70 ni watumiaji wa huduma hizo huku asilimia 10 imechangiwa na mfuko.

Sambamba na hilo amesema mpaka sasa mfuko umepeleka vifaa vya Tehama katika shule zaidi ya 500 ambapo kila shule ilipata kompyuta tano na printa moja kwa wastani.

No comments:

Post a Comment