MKUU wa Mkoa wa Mara, Adam Kighoma Malima amemtaka Meneja Mkuu wa Kampuni ya Acacia ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime kuwasilisha mara moja taarifa za jumla ya miradi ya kijamii uliyotekeleza katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo vilivyoingia mkataba nao ili kubaini utekelezwaji wa sheria inavyowataka.

Malima alitoa kauli hiyo alipokuwa katika ziara yake mapema wiki hii alipokutana na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime baada ya kupokea taarifa ya kamati yake iliyokagua na kutoa mapendekezo yake katika fedha zilizopokelewa na halmashauri hiyo kutoka katika eneo la tozo la ushuru wa huduma ‘service levy’ na kutumika sehemu ya mapato ya ndani ya miaka mitatu na nusu iliyopita.

Alimtaka meneja mkuu huyo wa mgodi atekeleze agizo hilo la Serikali kujua kiasi cha fedha kilichotumika kwenye miradi yote tangu mgodi huo uanze kuzalisha dhahabu mwaka 2000 kumuwezesha mkuu huyo kutofautisha na ile miradi ya maendeleo iliyoingia mikataba ya Vijiji vya Nyamwaga, Kerende, Nyangoto, Kewanja na Genkuru mwaka 1995.

“Nilimtaka Meneja Mkuu wa ACACIA wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara aniwasilishie taarifa ya miradi yote ya kimaendeleo katika vijiji vya mgodi huo iliyotekelezwa na mgodi huo kutoka fedha za service levy kwa mara ya pili tena kwani ni muda mrefu nilimtaka afanye hivyo alibakia kuchengachenga,” alisema Malima.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa Mkoa wa Mara aliutaka mgodi huo uhakikishe unaipatia jamii inayozunguka mgodi huo maji safi na salama ili kuwaepushia madhara ya kuendelea kunywa maji machafu.

“Mimi mwenyewe wakati ninafanya ziara yangu Wilaya ya Tarime nikielekea katika Wilaya ya Serengeti, nilishuhudia kina mama wakichimbua sehemu moja ili wapate maji, nilipowauliza wanahitaji maji hayo wafanyie nini walisema wanakwenda kuyatumia kwa kunywa na kupikia vyakula, nilishangaa sana kwani maji niliyoyaona wakiyachota ni machafu sana,” alisema Malima.

Hatua hiyo ilikuja baada ya baadhi ya wananchi kulalamika kutumia maji machafu kutokana na kuchanganyika na yanayotoka mgodini na kusababisha wengine kuugua baada ya kuyatumia.
Mtu mmoja anadaiwa kufa kutokana na maji hayo yanayotoka katika vyanzo vyao vya maji vilivyochafuliwa. Mtu huyo ni Bhoke Debora Marwa Byanda wa Kitongoji cha Nyamichale, Kijiji cha Nyakunguru, Tarime.

Wagonjwa wengine wanaougua kutokana na maji hayo ni Esther Mwita Mugusuhi wa Kitongoji cha Kwinyunyi katika Kijiji cha Matongo, Boazy Isaroche Range wa Kitongoji cha Shuleni Senta, Anastazia Mwita wa Kitongoji cha Masinki katika Kijiji cha Nyabichune na Maswi Nyaisanga wa Kitongoji cha Masinki katika Kijiji cha Nyabichune.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Apoo Castro Tindwa alisema baada ya kupata takwimu halisi za watu waliopata madhara ya maji hayo waliopo hai na waliofariki dunia na hasara ya mifugo iliyokufa kutokana na maji hayo, wataufungulia mgodi huo madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: