Tuesday, 16 April 2019

DR BASHIRU :CCM SIO CHAMA CHA UCHAGUZI TU BALI MAENDELEO YA WATUKATIBU  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dk Ally Bashiru amesema kuwa kama CCM itashindwa kusimamia misingi ya  haki na usawa kwa  wananchi , ikatetereka na kukumbatia watu  wanaotenda dhuruma, Ccm haitakuwa na haki ya kuongoza nchi.

Katibu mkuu huyo alisema hayo Leo wilayani  Kilosa wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za wilaya na mkoa wa Morogoro, pamoja na Viongozi na wananchi wa kata 9 za wilaya ya Kilosa .

‘’ Ni bora tukapigwa katika chaguzi kama tutashindwa kusimamia misingi ya haki na usawa kwa wananchi wetu,

‘’ Kazi ya CCM sio tu kupigiwa kura bali pia ni kusimamia  haki na usawa kwa wananchi wetu, tukishindwa kufanya hivyo hatutakuwa na sababu  ya kuongoza nchi hii’’alisema

Alisema  ni lazima kuchagua viongozi wenye  uwezo wa kusimamia haki na  masali ya wananchi wake kuliko wale wanaotanguliza maslai yao binafsi.

‘’ Chama hiki sio cha uchaguzi tuu , ni chama cha kutetea maslahi ya wananchi wake, kama kila kiongozi atatekeleza wajibu wake kwa kufanya hayo nchi yetu itasonga mbele kwa kasi kubwa’’ alisema Dk Bashiru,‘’ Tunataka kubadilisha nchi kutoka katika zama za giza kwa wenye nacho kuwadhalilisha wasio nacho, hatuwezi kuruhusu watu wajilimbikizia mali  bila kuhojiwa walizipataje’’ alisema.

Alisema kila mtu mwenye mali ni lazima ijulikane alizipata wapi na kama ni kwa njia ya halali hata akiwa tajiri vipi.

Aidha alisema wapo baadhi ya viongozi  na watumishi wamekuwa na macho ya gundi, kwa maana ya rushwa ambao wamekuwa wakisababisha kupoteza haki za wanyonge na kwamba CCM haiwezi kuwafumbia macho watu kama hao.

‘’ Wote tukizuia macho yetu kuwa na gundi , kuzuia rushwa nchi yetu itakuwa ya haki  na kila mmoja atakuwa sawa na mwingine hata akiwa tajiri anayelala ghorofani na anayelala katika nyumba ya chini’’ alisema.

Alisema wote wenye tabia hiyo hawatatoka salama na kwamba ni bora kila mmoja akaondoa gundi hiyo ili afanya kazi zake kwa haki na anayeshindwa ni bora akatafuta kazi ya kufanya.

‘’ Naambiwa nakuja kila wakati  Kilosa,  Kilosa ndio inaongoza kwa migogoro ya ardhi, hivyo kupitia  CCM ujumbe huu wa haki na usawa katika ardhi uweze kufikia nchi nzima kupitia Kilosa’’alisema.

Hata hivyo alisema wizara ya Ardhi imetenga fedha kwaajili ya kuhakiki mipaka na kutatua migogoro ya ardhi wilayani Kilosa na kwamba zoezi hilo lifanyike kwa uwazi na sio kwa siri.

Alisisitiza wataalamu kuzingatia maoni ya wananchi na kuyaweka kitaalamu   ili iweze kusaidia katika kutataua migogoro hiyo badala ya kuhalalisha uovu katika ardhi hiyo.

‘’ Hati sio msahafu,  kila hati zitachunguzwa  ili kujua uhalali wake ,wapo watu wana hati tena wanamiliki mashamba makubwa ambayo hayaendezwi huku wananchi wakihangaika kwa kukosa ardhi, mashamba kama hayo ni lazima  lazima yapelekwe kwa Rais ili aweze kuyafuta ili yarudi kwa wananch’’ alisema.

Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Shaka Hamdu Shaka alisema wapo baadhi ya viongozi ambao sio waaminifu na hawana nia njema na CCM wanatumia mwamvuli wa CCM kuficha maovu yao.

‘’ Viongozi hawa wamekuwa wakitishia kwamba CCM itashindwa kutokana na mambo yao , tunakuhakikishia katibu mkuu hatoka tayari kuwalea watu kama hawa ni bora tukashindwa katika chaguzi lakini sio kuwafumbia macho watu hao’’ alisema Shaka.

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Adam Mgoi alisema kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya pamoja na kamati ya siasa ya wilaya tayari imeshawabaini baadhi ya viongozi wanaosababisha migogoro ya ardhi kwa kuuza ardhi hizo kinyume na taratibu na kwamba watawachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

‘’Wapo baadhi ya wenyeviti wa vijiji na kata  ndio chanzo kikubwa cha migogoro hiyo, na sasa tutawashughulikia bila woga’’ alisema Dc huyo.Katika wilaya ya Kilosa yapo mashamba zaidi ya 190 makubwa na pori  ambapo hadi sasa ni mashamba 11 tu ndio yamefutiwa hati zake huku mengine yakiwa katika mchakato wa kuhakikiwa na kufuata taratibu za kuomba kufutiwa hati ambazo zitabainika kuwa hazina sifa.

No comments:

Post a comment