Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Aprili 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) bungeni leo tarehe 16 Aprili 2019 mara baada ya kujibu maswali ya wabunge wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akifuatilia mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma leo tarehe 16 Aprili 2019. Kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mkoani Tanga Mhe Rashid Abdallah Shangazi.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo – Dodoma

Serikali imeelekeza biashara ya zao la kahawa na mazao mengine kufanyika kupitia vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) badala ya wanunuzi kwenda kwa wakulima moja kwa moja. 

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 16 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini Mhe Martin Msuha aliyetaka kufahamu kwanini Serikali ilibadilisha mfumo wa ununuzi na uuzaji kahawa kwamba ni lazima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi pia ni vyama vingapi vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vimeundwa Wilayani Mbinga kufuatia kubadilishwa kwa mfumo huo.

Alisema kuwa utaratibu huo utamuwezesha mkulima kunufaika na kilimo cha kahawa kwa kuzalisha kahawa yenye ubora na kuuzwa kupitia minada ambapo wanunuzi watashindanishwa na hivyo kupelekea mkulima kupata bei nzuri na yenye tija.

Mhe Mgumba alisema kuwa Vyama vya Ushirika huanzishwa na wananchi kutokana na mahitaji yao hivyo, kupelekea kuwepo kwa aina mbalimbali za Vyama vya Ushirika kama vile Vyama vya Ushirika wa kilimo na masoko, mifugo, uvuvi, viwanda, nyumba, fedha na madini. Kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika Na.6 ya Mwaka 2013.

Kadhalika, alisema hadi sasa mkoa wa Ruvuma una jumla ya Vyama vya Ushirika vya msingi (AMCOS) vya kahawa 67 na chama Kikuu cha Ushirika kimoja (MBIFACU) ambavyo vimeanzishwa na wakulima wa kahawa katika Mkoa wa Ruvuma. Aidha, Wilaya ya Mbinga ina jumla ya Vyama vya Ushirika vya msingi vya kahawa 58 ambavyo ndio vitasimamia na kuendesha biashara ya kahawa katika Wilaya ya Mbinga.

Akijibu swali la Mhe Conchesta Rwamilaza ambaye ni Mbunge wa Viti maalumu kuhusu mradi wa kujenga masoko eneo la Nkwenda na Murongo katika Wilaya ya Kyerwa, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba alisema kuwa Masoko ya Nkwenda na Murongo katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa ni kati ya masoko matano (5) ya kimkakati yaliyopangwa kujengwa kupitia mradi wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Wilayani (District Agricultural Sector Investment Project – DASIP) na ujenzi ulioanza kutekelezwa mwaka 2006/07 hadi mwaka 2014.

Alisema masoko mengine yapo katika Halmashauri za; Busoka (Kahama), Kabanga (Ngara) na Sirari (Tarime). Mradi huo uligharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania.

Mhe Mgumba alisema kuwa lengo la ujenzi wa masoko hayo ya kimkakati ilikuwa ni kuanzisha mfumo thabiti wa masoko utakaongeza tija na pato kwa wakulima ndani ya Wilaya.

Alisema kuwa mfumo huo utajenga mazingira wezeshi kibiashara katika maeneo ya mpakani ili kurahisisha biashara na nchi jirani na kuinua hali za kiuchumi za wananchi wa maeneo hayo na uchumi wa Taifa kwa ujumla.  

Alisema hadi sasa mradi wa DASIP unafungwa Disemba 2013/14 kazi ya ujenzi wa masoko hayo ilikuwa haijakamilika na yalikuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Kwa kuzingatia umuhimu wa masoko hayo ya kimkakati katika Halmashauri husika, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa masoko hayo na mengine nchini kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambapo katika bajeti ya mwaka 2019/2020 Serikali imetenga Shilingi bilioni 2.9 kuendelea na ujenzi wa masoko hayo.

MWISHO.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: