Taasisi zinazohusika na Masuala ya TEHAMA nchini zimetakiwa kuendelea kushirikiana katika kuinua vipaji vya wanafunzi wanaosoma masomo yahusuyo TEHAMA na kuviendeleza ili viweze kuondoa changamoto zilizopo katika jamii.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akifunga mafunzo na mashindano ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA yaliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote.

Prof. Ndalichako amesema kuwa nia ya Serikali ni kuona mchango wa Sayansi na Teknolojia ukiongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za jamii na kuongeza tija katika uzalishaji hususani katika sekta zinazogusa wananchi moja kwa moja zikiwemo za uchumi, kilimo, mifugo na viwanda.

"Hadi sasa tunaona mafanikio mengi ya matumizi ya TEHAMA ambapo hata wajasiriamali wamekuwa wakikuza biashara zao kupitia mitandao, pia mapato ya serikali yameendelea kuongezeka baada ya kuingia kwenye mfumo wa matumizi ya TEHAMA hivyo kutokana na mafanikio hayo, natoa rai kwa wadau wote wa TEHAMA kushirikiana na Serikali sio tu kuinua vipaji bali na kuviendeleza,” alisema Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amefafanua kuwa Serikali imeendelea kutoa msisitizo katika masuala ya TEHAMA ambapo hivi karibuni imetoa  jumla ya Kompyuta 300 na Projekta 100 kwa ajili ya kuendeleza mafunzo ya teknolojia, habari na mawasiliano kwenye Vyuo vya Walimu pia zimeanzishiwa maabara za kompyuta kwa baadhi ya shule ili kuendeleza mafunzo ya teknolojia hiyo.

Ametoa rai kwa wanafunzi kuacha kuitumia vibaya TEHAMA na badala yake kusoma masomo hayo kwa kuwa fursa za masomo ya Sayansi na Teknolojia ni nyingi pia zinatoa nafasi kwa watu kujiajiri kwa kutengeneza programu mbalimbali ambazo zinaweza kuuzwa kwa gharama kubwa.

Akiongelea kuhusu mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, (UCSAF) Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA ilianzishwa kwa lengo la kumuhamasisha mtoto wa kike kuchagua masomo ya TEHAMA na kuweza kupata fursa katika sekta hiyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: