Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua rasmi mpango wa kutambua na kusajili kila kipande cha ardhi kwa Mkoa wa Dar es Salaam kama sehemu ya kuongeza usalama wa milki ya ardhi.

Kupitia mpango huo wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wote watatambuliwa na kisha kupewa leseni ya makazi au hati ya makazi ambayo itakuwa katika mfumo wa kieletroniki.

Akizungumza leo Machi 16,2019 wakati wa uzinduzi wa mpango huo ambao utaanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam na kisha kuendelea mikoa yote nchini, Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema leseni hiyo baada ya kutolewa itadumu kwa miaka mitano.

“Ndani ya hii leseni ya kieletroniki ambayo itadumu kwa miaka mitano kutakuwa na taarifa zote muhimu.Kutakuwa na jina la mmiliki wa ardhi, ukubwa wa kiwanja, majirani zake, namba za kitambulisho cha Taifa na taarifa nyingine muhimu.

“Kwa hiyo leseni hiyo ya makazi itawezesha kila kipande cha ardhi kutambuliwa kikamilifu, hata ukiwa nje ya Tanzania kiwanja kitaonekana maana kipo kieletroniki.

“Tutaondoa changamoto za ujambazi wa viwanja lakini pia wakati huo huo leseni ya makazi itasaidia katika kupata mkopo benki na leseni hii itarahisisha masuala ya ulinzi na usalama,”amesema Lukuvi.

Amesema kila mwananchi atatakiwa kuchangia Sh.5000 ambapo Sh.4000 zitakwenda katika manispaa na Sh.700 itakwenda kwa kijana ambaye ni mtaalama anayetembea na simu kwa ajili ya kufanya usajili huo na Sh.300 zitakwenda kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ambaye atakuwa na mtaalam husika.
Share To:

Post A Comment: