Na WAMJW-DOM.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali imefanukiwa kuokoa kiasi cha Shilingi Bilion 3.4 ambacho kingetumika katika matibabu kwa Wagonjwa wa Figo nje ya Nchi.
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo leo Machi 14 wakati akiongea na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma ikiwa ni Siku ya Figo Duniani ambayo inaongozwa na kauli mbiu ya Afya ya figo kwa kila mmoja kila.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali imeokoa kiasi cha shilingi bilioni 4.2 ambacho kingetumika katika matibabu ya wagonjwa 80 mpaka 100 ambao wangepelekwa nje ya nchi kwaajili ya matibabu.
“Wagonjwa waliokwishapandikizwa figo hapa nchini ni 42, kama tungewapeleka  wagonjwa nje ya nchi ingegharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni 4.2 kwa idadi hiyo ya wagonjwa.  80 mpaka 100, wakati huduma hii hapa nchini inagharimu kiasi cha shilingingi milioni 21 kwa kila mgonjwa.” Alisema Dkt. Ndugulile
Aidha, Dkt, Ndugulile amesema kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia magonjwa ya figo ni pamoja na uzito wa kupindukia (obesity), matumizi makubwa ya sigara, unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara,kutokufanya mazoezi na kunywa madawa kiholela hasa dawa za kupunguza maumivu.
Aliendelea kusema kuwa, magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu ni magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha matatizo ya figo, magonjwa haya yakitambuliwa mapema yanaweza kudhibitiwa kwa matibabu na kuepusha madhara kwenye figo.
Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile amesema kuwa Kufikia Desemba mwaka 2018, jumla ya vituo 28 vyenye jumla ya wagonjwa 1050 vilikuwa vikitoa huduma ya usafishaji damu katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma.
Mbali na hayo, Dkt. Ndugulile amesema Serikali imepiga hatua kubwa ya kuanzisha huduma za kupandikiza figo hapa nchini katika hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Figo nchini Dkt. Onesmo Kisanga amesema kuwa Ugonjwa wa Figo ni tatizo kubwa nchini huku wananchi wengi wakiwa na uelewa mdogo juu ya athari na visababishi vya ugonjwa huo.
Aidha Dkt. Onesmo amewataka wananchi kuacha tabia ya kunywa dawa bila kupata ushauri wa kitaalamu hivyo kuepuka kuzalisha sumu mwilini na kupelekea ugonjwa wa figo.
Hata hivyo Dkt. Onesmo Kisanga ameishukuru Serikali kwa kuwaendeleza kimasomo wataalam kwenye upande wa matibabu ya figo ambao sasa wamesambazwa sehemu mbali mbali ndani ya nchi kutoa huduma za matibabu.
Naye Dkt. Grace Maghembe Kaimu Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya amesema ungojwa huu umekuwa ukiwaathiri zaidi wakazi wa mijini kuliko vijijini kutoka na mfumo wa maisha uliopo sasa ambapo watu wengi wamekuwa hawazingatii mtindo bora wa maisha kwa kutofanya mazoezi pamoja na kula chakula bora.
Dkt. Maghembe amesema bado ipo changamoto kwenye matumizi ya dawa za mitishamba ambazo bado hazijatambuliwa na kuthibitishwa huku akiwataka wananchi kuwa waangalifu pia kwenye matumizi ya dawa hizo.
“Serikali inatambua umuhimu wa tiba mbadala pamoja na matibabu ya tiba za asili na ndio maana zipo taasisi za serikali zinazohusika kuzitambua dawa hizo ni zipi na zina vitu gani na unatakiwa kutumia kwa kiwango gani” amesema Dkt Maghembe nakuwataka watengenezaji wa dawa hizo kufuata taratibu zilizopo ili kuthibitisha na kusajili dawa zao.
Share To:

Post A Comment: