Serikali kupitia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la polisi kuwatumia Wafungwa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na madarasa ya Chuo cha Taaluma ya Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Masauni, aliyasema hayo jana wakati alipotembelea majengo chakavu ya chuo hicho na kubaini kati ya fedha hizo zilizotolewa sh.millioni 700 kiasi cha Sh. milioni 200 zimetengwa kulipa vibarua watakao shughulikia ujenzi huo.

Desemba 21, mwaka jana, Rais Magufuli wakati wa hafla ya kutunuku vyeo wahitimu 515 waliofanya vizuri zaidi mafunzo ya uofisa wa ukaguzi, aliahidi kutoa Sh. milioni 700 ili zisaidie ujenzi huo.

Kutokana na hali hiyo Masauni aliliagiza Jeshi la Polisi badala ya kutumia Sh. milioni 200 kulipa vibarua watakaotumika kwenye ujenzi huo, fedha hizo zielekezwe kwenye mambo mengine.

Mhe. Hamad Masauni alisema wizara yake ina taasisi ya Magereza ambayo ina nguvu kazi ya kutosha, hivyo Jeshi la Polisi liwasiliane na magereza ili waweze kutumia wafungwa kwenye ujenzi huo badala ya vibarua.

"Rais alishaagiza wafungwa watumike katika shughuli za uzalishaji, sioni sababu ya kutumia fedha hizi kuwalipa vibarua wa nje, naagiza muwasiliane na Jeshi la Magereza pamoja na kikosi cha ufundi kilichopo ndani ya Jeshi la Polisi ili kuona namna ya kuokoa fedha hizi," alisema naibu Waziri.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Naibu Kamishna Anthony Rutashuburugukwa, alisema majengo yatakayojengwa ni ghala la chuo, madarasa matatu, bweni moja la askari wa kiume na lingine la askari wa kike.
Share To:

Post A Comment: