Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka watumishi wa Wakala wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) kutumia taaluma yao kubuni mbinu zitakazovutia taasisi za umma, sekta binafsi na watanzania kwa ujumla kupenda kutumia mifumo ya TEHAMA ili kuiongezea Serikali mapato na kupunguza gharama.

“Mkiwa kama wataalam wa masuala ya mawasiliano kwa njia ya video na mafunzo kwa njia ya mtandao, jaribuni kusumbua akili zenu kwa kuweka njia madhubuti zitakazowavutia watanzania kupenda wenyewe kutumia mawasiliano kwa njia ya video na mafunzo kwa njia ya mtandao ili kuendana na teknolojia na kupunguza gharama,” Amesema Mary.

Akizungumza na watumishi wa Wakala wa Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) alipofanya ziara ya kikazi katika wakala huo, Mary amesema ni lazima watumishi wa Wakala huo wafanye kazi zenye matokea chanya ambazo zitapunguza gharama kwa serikali kama ambavyo Rais  Dkt. Magufuli anasisitza.

“Ni lazima tujue kiongozi wetu Mkuu wa Nchi anataka nini katika utendaji kazi wetu, tufanye kazi kwa bidii na kuipunguzia serikali gharama zisizokuwa za lazima,” Dkt. Mary ameongeza.

Aidha, amewapongeza watumishi wa wakala huo kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuangalia namna bora ya kujitangaza ili kufahamika na kupata wateja wengi watakaotumia mawasiliano kwa njia ya video na mafunzo kwa njia ya mtandao ili kuiongezea serikali mapato.

Aidha, ameahidi kutoa ushirikiano kwa watumishi wa wakala huo katika kutekeleza majukumu yake na kuboresha utuoaji huduma kwa umma.

Katika ziara hiyo, Dkt Mary ameshuhudia teknolojia ya mawasiliano kwa njia ya video kwa kuunganishwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Nairobi, Kenya na ofisi yake jijini Dodoma.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: