Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akiwasili katika Ofisi ya Wilaya ya Hai, alipofanya ziara ya kutatua mgogoro kati ya Mwekezaji wa kilimo cha kahawa kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes na Vyama vya Ushirika vya kilimo hicho wilayani  Hai (Murososangi). Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Hai Bw. Lengai Ole Sabaya.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wawekezaji na Wanachama wa  Ushirika wa kilimo cha zao la Kahawa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro (Murososangi).
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghwira, akizungumza na wadau wa kilimo cha Kahawa wilayani Hai wakati wa  mkutano kati Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki (hawapo pichani) na wadau wa kilimo cha kahawa wilayani Hai.
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia) wakisikiliza kwa makini maelezo ya  wanaushirika wa kilimo cha Kahawa wilayani Hai- Murososangi, kuhusu kiini cha mgogoro na Mwekezaji wa Kampuni ya Tudeley Estates Limited  kutoka Uingereza  kuwa ni kuletwa kwa Mwekezaji mwingine kutoka Ujerumani Bw. Marcus Shiber, bila ridhaa yao.
Wanaushirika wa kilimo cha Kahawa wilayani Hai- Murososangi, wakiwa katika Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki (hawapo pichani) walipofika wilayani hapo kutatua mgogoro ya uwekezaji katika zao la kahawa.
Mwekezaji wa Kilimo cha Kahawa kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahawa ya Mbosho Bw. James Powell wakiwa katika mkutano wa kutatua mgogoro ya uwekezaji katika zao la kahawa chini ya uenyekiti wa  Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), na kuwashirikisha Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki (Mb) (hawapo pichani) na wadau wa kilimo cha kahawa Wilayani Hai.
Wadau wakiwa katika  mkutano wa kutatua migogoro kati ya wawekezaji na Chama cha Ushirika wa wakulima wa Kahawa Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghwira (kulia) akipeana mkono na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) alipofika wilayani Hai, kutatua mgogoro ya wawekezaji katika Sekta ya kilimo cha kahawa katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Na Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Kilimanjaro
Serikali  imeitaka Kampuni ya Tudeley Estates Limited  kutoka Uingereza  iliyoingia mkataba na vyama vya Ushirika Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro vinavyojishughulisha na uwekezaji wa Kilimo cha Kahawa (Murososangi), kurudi nchini ili kufanikisha utatuzi wa mgogoro uliosababishwa na kuibuka kwa mwekezaji mpya ambae mkataba wake haujulikani.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angela Kairuki walipofanya mkutano na Wawekezaji, Vyama vya Ushirika na Wadau wengine kuhusu mgogoro na Mwekezaji huyo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Mpango alisema kuwa, Vyama vya Ushirika vya Murososangi, viliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited ya nchini Uingereza ambapo washirika hao wenye mashamba eneo la Kibo na Kikafu  wilayani Hai, yenye ukubwa wa hekari 2054 walimpa Mwekezaji huyo ili kuendeleza zao la kahawa kuanzia mwaka 1998.
Alisema kuwa baada ya mwekezaji  huyo, Bw. Conrad Legg, kuonesha nia ya kutoendelea na uwekezaji huo aliondoka nchini, wakaja wawekezaji wengine kutoka Ujerumani ambao waliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited, kwa kununua hisa bila  kuvishirikisha Vyama vya Ushirika vilivyoingia mkataba wa awali jambo lililosababisha sintofahamu kwa wana ushirika hao.
“Aliyeingia mkataba na Murososange, arudi nchini ili kutatua mgogoro huo ili kuona Wananchi wanawezaje kuingia mkataba mwingine na mwekezaji mpya ambao utalinda maslahi ya wananchi wenye mashamba hayo na pia mwekezaji”, alisema Dkt. Mpango.
Alisema Wanaushirika hao wanataka Mwekezaji wa kwanza arudi nchini ili wavunje mkataba wa awali kwa kuwa mkataba huo haujaisha muda wake hivyo hawawezi kuingia mkataba na mwekezaji mpya wakati ule wa awali bado unaendelea.
Aidha, alisema kuwa mwekezaji mpya kutoka Ujerumanim Bw. Marcus Shiber,  alianza kuleta fedha katika eneo la uwekezaji  na kulipa baadhi ya kodi za mtangulizi wake, madeni, mishahara na kuboresha miundombinu ya mashamba hayo bila kupata muafaka na Vyama vya Ushirika jambo ambalo liliendelea kuleta mgogoro.
Dkt. Mpango alisema kuwa, wamepata maelezo kutoka pande zote na baadhi ya maelezo hayo yanahitaji ushauri wa kisheria hivyo tumeiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuyafanyia kazi mambo hayo ili kuweza kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, namna bora ya kumaliza mgogoro huo bila kuingizia Serikali hasara.
Aliwatahadharisha watendaji wakuu wa serikali kutotumia ubabe na vitisho kwa wawekezaji ili kutoharibu taswira ya taifa katika masuala ya uwekezaji unaopigiwa chapuo hivi sasa na Serikali ya Awamu ya Tano, ili kuvutia mitaji, mapato ya serikali, ajira kwa vijana na kuvutia teknolojia za kisasa kwa maendeleo ya Taifa.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki, alisema kuwa kutokana na mgogoro huo wa kiuwekezaji akaunti za Mwekezaji mpya kutoka Ujerumani ikiwemo ya Kampuni ya Kuza Afrika inayojishughulisha na kilimo cha parachichi Mkoani Mbeya ilifungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhusiana na masualaya kodi, jambo lililosababisha baadhi ya shughuli za Mwekezaji huyo kukwama.
Alisema kuwa kikosi chao kupitia Waziri wa Fedha na Mipango aliyetumwa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kutatua mgogoro huo, wameangalia iwapo taratibu za kufungwa akaunti hizo zilifuatwa na kutafuta njia bora ya kutatua tatizo hilo na pia kuona ni Mwekezaji yupi anafaa kuingia mkataba na Vyama vya Ushirika vya Murososangi, nia ikiwa ni kuona Vyama hivyo vinanufaika na Uwekezaji unakua nchini.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mgwira, aliishukuru Serikali kwa hatua yake ya kutuma Mawaziri ili kutatua mgogoro huo wa muda mrefu ambao utatuzi wake utasaidia Wananchi kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini-TIC, Bw. Geofrey Mwambe, alisema kuwa katika mkutano kati ya Mawaziri, Wawekezaji na Vyama vya Ushirika wamebaini kuwa utaratibu walioukuta Wawekezaji kutoka Ujerumani haukuwa sawa na ule ambao waliwekeana na Mwekezaji wa kwanza kutoka Uingereza, hivyo kuleta ugumu kiutendaji kwa Mwekezaji wa pili.
Alisema kuwa, Serikali inahitaji uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ili  kupata malighafi ya viwanda nchini, kuongeza mnyororo wa thamani na kukuza pato la Taifa, hivyo inafanya jitihadi za kuvutia wawekezaji watakaoleta mitaji na teknolojia ya kisasa ili Taifa liweze kukabiliana na ushindani wa bidhaa katika soko la Kimataifa.
Mwakilishi wa mwekezaji mpya kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuwatuma Mawaziri wake kuja kutatatua mgogoro huo, alisema Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hivyo yupo tayari kuendelea kuwekeza zaidi nchini kwa lengo la kupata manufaa kwa pande zote ikiwa ni pamoja na Kampuni yake na vyama vya ushirika wa kilimo cha Kahawa Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.
Share To:

Post A Comment: