Mgeni rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza umuhimu wa mbegu bora za kilimo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu, katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya, Tarehe 5 Machi 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
Sehemu ya washiriki wa uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) Tarehe 5 Machi 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu, katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya, Tarehe 5 Machi 2019.
Sehemu ya washiriki wa uzinduzi wa Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) Tarehe 5 Machi 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya

Uimarishaji wa mitandao ya usambazaji mbegu na viuatilifu ni muhimu katika kuhakikisha tija inaongezeka katika Uzalishaji wa mazao yote hususani nafaka, matunda mbogamboga na mbegu za mafuta.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 5 Machi 2019 wakati akizindua Mpango wa kuimarisha Mitandao ya Usambazaji wa Mbegu na Viuatilifu, Mpango unaotekelezwa na Mradi wa NAFAKA na Kampuni ya Kimataifa ya CORTEVA katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nchini Tanzania.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Usungilo Hoteli Jijini Mbeya Mhe Hasunga alisema kuwa kuimarisha usambazaji mbegu na viuatilifu utamsaidia mkulima kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza pato lake hivyo kuchangia katika kuipeleka Tanzania kufikia Uchumi wa Kati kama inavyoeleza sera ya Serikali ya awamu ya tano inayongozwa na Mhe Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Alisema wakulima nchini Tanzania wanategemea Sekta ya kilimo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi, kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 65 ya wananchi, ina uwezo wa kutoa malighafi ya viwanda kwa asilimia 66 na inachangia asilimia 100 ya chakula kinachopatikana.

Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya II yaani Agricultural Sector Development Program - ASDP II inaolenga kuleta Mapinduzi katika sekta ya kilimo.

Programu hiyo ya miaka kumi (10) imeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2018 na inafanyia kazi maeneo ya Usimamizi endelevu wa ardhi na maji, Kuongeza Tija (kuongeza matumizi ya pembejeo), Kuongeza masoko na kuongeza thamani ya mazao, Kuboresha mazingira ya uwekezaji katika kilimo. Hivyo, Uimarishaji wa Mpango wa Kusambaza Pembejeo na Viuatilifu ni moja ya shughuli muhimu katika Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo -ASDP 11 katika kuongeza tija. 

“Ni Imani yangu kuwa, kufanikiwa kwa kazi hii ya Mradi wa Nafaka ni kufanikiwa katika utekelezaji wa sehemu ya Programu ya Kuendeleza Kilimo nchini ASDP II. Mradi huu pia utaendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo baina na Serikali na Sekta nafsi katika kuendeleza kilimo nchini” Alisema

Kadhalika, Hasunga alisema Serikali inatambua mchango unaotolewa na Shirika la Misaada la Marekani USAID katika miradi mbalimbali husasani katika sekta ya kilimo. Mradi wa NAFAKA ni moja ya michango ya Shirika la USAID katika kuongeza tija kupitia Mashamba darasa, Uendeshaji wa Vikundi na vyama vya wakulima, Kuongeza thamani kwenye usindikaji wa Mahindi kwa njia ya virutubishi kwenye unga, Kuunganisha wakulima na huduma za kifedha Masoko na Bima ya Mazao yaani “Crop Insurance”.

Alisema kuwa Shughuli hizo zinazotekelezwa na Mradi wa NAFAKA kwa kushirikiana na CORTEVA  unaenda sambamba na jitihada za Wizara ya Kilimo katika kuendeleza kilimo. Moja ya maeneo ya kipaumbele yanayotekelezwa na Wizara ni kuongeza tija katika uzalishaji kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, na kuimarisha huduma za ugani.

Maeneo mengine ya Kipaumbele ya Wizara ya Kilimo ni Kutungwa kwa sheria ya kilimo ili kusimamia kilimo, Kuandikisha wakulima wote, Kuongeza uzalishaji wa sukari kuondoa upungufu wa sukari nchini, Kufungamanisha uzalishaji na mahitaji ya viwanda ili kutoa mali ghafi ya viwanda kwa kuongeza uzalishaji, Kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta, Kuanzisha scheme za umwagiliaji ili kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji, Wakulima kuwa na bima ya mazao, na Kuongeza fursa za upatakanaji wa fedha kwa wakulima.

“Ni jambo la faraja kuona sekta binafsi sasa zinatoa mchango katika jitihada za Serikali katika kutoa mafunzo kwa wakulima kwa kuanzisha mashamba darasa, kutoa mafunzo kwa maafisa ugani, kusimamia na kuhimiza matumizi ya mbegu bora na viuatilifu pamoja na kufanya kazi na mawakala wa pembejeo wa daraja la kati na wadogo waliopo vijijini wapatao” Alikariirwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Ni jambo la kutia moyo kuwa mpango huu utasaidia usambazaji na upatikanaji wa viuatilifu vya kupambana na visumbufu vya mlipuko vikiwemo viwavi jeshi vamizi “Fall Army Worms” katika maeneo yaliyovamiwa kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nchini mwetu”

Aidha, alisema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika kilimo ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio katika taratibu zilizowekwa katika uzalishaji, usambazaji na uingizaji wa mbegu ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima nchini.

Katika suala la soko la mahindi Serikali imesharekebisha suala hil0 na itaendelea kutoa taarifa za hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha taratibu za masoko ya mazao ili wakulima, wafanyabiashara na wadau waweze kunufaika na uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Sambamba na hayo pia Waziri Hasunga alisema kuwa serikali itaweka msisitizo katika sekta ndogo ya ardhi ili wakulima kuona umuhimu wake na kuondokana na kilimo kinachotegemea mvua.

Share To:

Post A Comment: