Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya wakulima wa Korosho wakati akizungumza katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019. (Picha zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya wakulima wa korosho Mkoani Lindi wakifatilia ufafanuzi wa malipo kutoka kwa Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akizungumza katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019. 
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe Godfrey Zambi akitoa maelezo ya awali kuhusu sekta ya kilimo, mifugo na maji mbele ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019. 
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakikagua mtambo wa kutengeneza kimininika cha Nitrojeni inayohifadhi Mbegu wakati wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019. 
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakikagua chanzo cha Maji na mfumo wa kutibu maji katika kijiji cha Ng'apa wakati wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019. 
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakikagua kiwanda cha kubangua Korosho katika eneo la Mnazimmoja  wakati wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Lindi

Serikali imewahakikishia wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa kufikia tarehe 31 Machi 2019 wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki umekamilika kwa kiasi kikubwa.

Hakikisho hilo mbele ya kamati hiyo limetolewa leo Tarehe 16 Machi 2019 na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi wakati akitoa ufafanuzi katika mkutano uliowakutanisha wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake Dkt Christine Ishengoma, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Naibu Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, wataalamu serikalini sambamba na wakulima.

"Kumekuwa na urasimu mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hili la uhakiki lakini sasa tumeamua kama serikali kabla ya mwisho wa mwezi huu wa tatu wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ili kuondoa adha wanazokumbana nazo" alikaririwa Mhe Hasunga

Alisema pamoja na kwamba malipo ni mchakato unaohitaji kupitia katika hatua nyingi za mchakato ikiwemo uhakiki lakini kila jambo lenye mwanzo ni lazima kuwa na ukomo.

Alisema mpaka sasa Tani 222,684 zimekwisha kusanywa huku hadi kufikia tarehe 14 Machi 2019 tayari jumla ya Shilingi Bilioni 596.9 zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya Shilingi Bilioni 723

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amewahakikishia wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa pamoja na mchakato huo wa malipo ya Korosho kuendelea lakini pia Wizara imepitia katika michakato mbalimbali ya kumpata Mkurugenzi mpya wa Bodi ya Korosho ili kuendelea na majukumu ya Bodi hiyo.

Kuhusu wanaofanya biashara ya zao hilo kinyume na sheria maarufu kama Kangomba Waziri Hasunga alisema kuwa tayari serikali imewabaini na wote watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia Pembejeo feki Mhe Hasunga alisema kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kwa wafanyabiashara wote waliofanya hujuma kwa kuwauzia wakulima Mbegu na mbolea feki ambapo hatua kali zimeanza kuchukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutolipwa fedha wanazodai kwa kusambaza Pembejeo hizo.

Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameuagiza uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa viuatilifu Vya Tropiki (TPRI) kutuma wataalamu Mkoani Lindi ili kuchukua sampuli za viuatilifu kwa wakulima na kuvipima ili kubaini kadhia ya usambazaji wa viuatilifu feki kwa wakulima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Dkt Christine Ishengoma (Mb) amemuagiza Waziri wa Kilimo kuhakikisha kuwa taarifa ya malipo ya wakulima wote wa Korosho inafika bungeni tarehe 2 Aprili 2019.

MWISHO
Share To:

Post A Comment: