Wednesday, 6 March 2019

MHE HASUNGA AANZA ZIARA JIMBONI VWAWA, ASISITIZA ULAZIMA WA UPATIKANAJI WA MBOLEA KWA WAKATI

Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye pia ni waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika Kijiji na Kata ya Nanyala katika ziara yake ya siku tano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi iliyoanza jana tarehe 5 Machi 2019.(Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya wakazi wa Kijiji na Kata ya Nanyala wakifatilia mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye pia ni waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga jana tarehe 5 Machi 2019.
Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye pia ni waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika Kijiji na Kata ya Nanyala katika ziara yake ya siku tano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi iliyoanza jana tarehe 5 Machi 2019.
Sehemu ya wakazi wa Kijiji na Kata ya Nanyala wakifatilia mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye pia ni waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga jana tarehe 5 Machi 2019.

Na Mathias Canal, Songwe

Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye pia ni waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga jana tarehe 5 Machi 2019 ameanza ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Katika ziara hiyo iliyoanzia katika Kijiji na Kata ya Nanyala Mhe Hasunga amesisitiza ulazima wa mbolea kuwafikia wakulima kwa wakati kuanzia msimu huu wa kilimo wa mwaka 2019/2020

“Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita Mbolea ilikuwa ikiishia Jijini Dar es salaam badala ya kuwafikia wakulima jambo hilo tumelikataa ni lazima mbolea ifike kwa wakulima kwa wakati” Alikaririwa na kuongeza kuwa

“Ni jambo la kushangaza kuona mbolea nyingi inawekwa Dar es salaam wakati hakuna uhitaji mkubwa wa mbolea sasa naagiza mbolea yote kuwafikia wakulima ili kurahisisha huduma za kilimo”

Mhe Hasunga pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa Wizara ya Kilimo imejipanga kuhakikisha kuwa masoko ya mazao mbalimbali yanapatikana ili kurahisisha na kuongeza ufanisi wa kipato kwa wakulima.

Alisema kuwa wakulima wamekuwa wakitumia nguvu nyingi katika kilimo lakini masoko ya mazao yao yanakosekana na katika kulikabili hilo wizara imeanzisha kitengo maalumu kitakachoshughulikia masoko.

Alisema katika kutekeleza hatua za utafutaji masoko Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli tarehe 4 Januari 2019 alishuhudia utiaji saini mkataba wa mauziano ya Tani 36,000 za mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la chakula Duniani (WFP).

“Kuna Taasisi zangu zinazoshughulika na ununuzi wa mazao ya wakulima ambazo ni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya nafaka na Mazao mchanganyiko, tumezielekeza kuhakikisha zinanunua mazao mengi ya wakulima kwa kufanya hivyo tutaimarisha soko la wakulima” Alisema

Katika hatua nyingine Mhe Hasunga amewapongeza wakulima katika Jimbo la Vwawa na Mkoa wa Songwe kwa ujumla wake kwa kujihusisha na kilimo kwa asilimia kubwa huku akisisitiza ulazima wa kuongeza tija katika kilimo kwa kutumia wataalamu mbalimbali.

Mhe Japhet Hasunga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Vwawa na Waziri wa Kilimo ameanza ziara ya siku tano Jimboni humo ambapo atakutana na wapiga kura wake akiwa na dhamira ya kutatua changamoto zao.

No comments:

Post a Comment