Na Mwandishi Wetu, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amefanya ziara ya kushtukiza kituo cha Askari wa Usalama Bararani (Trafiki) Buigiri Mkoani Dodoma, baada ya kupokea malalamiko mara kwa mara kutoka kwa madereva wanaoitumia barabara hiyo.

Lugola alifika katika kituo hicho kilichopo barabara kuu ya Dodoma-Morogoro, nje kidogo ya Jiji la Dodoma, jana saa kumi alasiri akiwa ameambatana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani humo, SSP Nuru Selemani, na kuanza kutaka kujua utendaji kazi wa askari hao katika kituo hicho.

Akizungumza na askari hao, Lugola aliwataka wafanye kazi kiweledi bila kuwaonea madereva kwa kuwaomba rushwa au kuwapiga faini kwa uonevu.

“Licha ya kuwapongeza kwa kazi nzuri kwa kuyaongoza magari lakini mnapaswa kufuata sheria na si kufanya kazi kwa uonevu, nimekua napokea malalamiko mara kwa mara kutoka kwa madereva kuhusu kituo hiki, fanyeni kazi kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani zinavyoelekeza,” alisema Lugola.

Kwa upande wake SSP Selemeni, alimweleza Waziri huyo kuwa, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utendaji wa kazi zao, lakini maelekezo ya utendaji kazi wa weledi waliopewa wameyapokea na kuahidi kuyafanyia kazi.

Lugola alisema yeye ni Waziri ambaye anafuatilia maagizo yake kila anapoyatoa, hivyo askari ambao wanachafua Jeshi la Polisi hatawavumilia, na ataendelea kufanya ziara za kushtukiza kama hizo mara kwa mara sehemu mbalimbali nchini.

Waziri huyo yupo njiani kuelekea Mjini Morogoro kwa ajili ziara ya kikazi atakayoifanya Kesho Machi 15, Tarafa ya Kimamba, Wilayani Kilosa, Mkoani humo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: