Na. Vero Ignatus, Dar

Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama imezinduliwa leo Jijini Dar es salaam na mkuu wa mkoa huo Mhe. Paul Makonda yenye lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Mhe. Makonda amezipongeza huduma zinazotolewa na watoa huduma za afya, huku akiwataka wanaume kuwasindikiza wake zao Kliniki ili waweze kupata taarifa zitakazowasaidia wake zao kujifungua salama.

 “Nimejaribu kupita kwenye wodi mbalimbali napata matumaini kwamba wagonjwa wanapata huduma bora. Nawapongeza watoa huduma za afya, naomba waendelee hivyo hivyo.” alisema Makonda.

Amepongeza  jitihada za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. John Pombe Magufuli katika jitihada za kuboresha huduma za afya ambapo amesema kuwa tayari mkoa wa Dar es salaam umeshapata pesa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika wilaya mbili na tayari ujenzi wa wodi ya mama na mtoto umeanza katika wilaya ya Kinondoni, Temeke ikifuatia.

“Mhe. Rais ametoa pesa hizi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya zikiwemo huduma za afya kwa mama na mtoto ili kuwawezesha akina mama kujifungua salama.” alisema

Aidha  ametoa  wito kwa wananchi kujitokeza kutoa damu salama ili kupunguza vifo vya akina mama na vifo vitokanavyo na uzazi sambamba na taasisi, mashirika mbalimbali kusaidia kuwezesha upatikanaji wa huduma za haraka kama vile za kusaidia watoto njiti.

“Sekta ya afya hususani kwa mama na mtoto inahitaji mchango na ushiriki wetu sote, ofisi yangu itahakikisha bajeti ya 2019/2020 inaongezeka katika sekta hii ili kuweza kufikia malengo ya kumvusha mama na mtoto salama.” Alisema Makonda.

Ziada Sela ni mratibu wa afya ya mama na mtoto amesema  kuwa kampeni imejikita katika mambo tisa ili kuhakikisha mama na mtoto wanavuka salama, ambayo ni pamoja na huduma rafiki kwa vijana, elimu pamoja na ushauri nasaha na vipimo, huduma za dharura kwa matatizo ya uzazi na damu salama.

Ameongeza  kuwa mambo mengine ambayo wamejikita nayo ni pamoja na ushirikishwaji wa jamii, kutoa taarifa ya kila kifo kinachotokana na uzazi ili kujua tatizo na kulipatia suluhisho, upatikanaji wa huduma kwa watoto wachanga, huduma ya rufaa pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma.

Kwa upende wao wakuu wa wilaya za Kigamboni, Temeke na Ilala za mkoa wa Dar es salaam walisaini ahadi za kutekeleza kampeni hiyo katika wilaya zao ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.

Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ni kampeni ya kitaifa inayolenga kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga na ilizinduliwa rasmi na Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan mwezi Novemba mwaka 2018

Pia imeshazinduliwa katika ngazi za mikoa ikiwemo katika mikoa ya Lindi, Tabora, Dodoma, ambapo Kampeni hiyo  inatekelezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo UNICEF.
Share To:

Vukatz Blog

Post A Comment: