Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana Jumatatu tarehe 11 hadi 31 Machi, 2019 Mjini Dodoma kutekeleza majukumu ya kibunge kabla ya Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 02 Aprili, 2019.  Kwa mujibu wa Ratiba ya Shughuli za Kamati, Waheshimiwa Wabunge wote wanapaswa kuwasili Mjini Dodoma Jumapili tarehe 10 Machi, 2019 tayari kwa ajili ya kuanza kwa vikao vya Kamati. 

Shughuli zitakazotekelezwa na Kamati hizo ni pamoja na:

KUPOKEA WASILISHO LA SERIKALI KUHUSU KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI

Katika kipindi hicho cha vikao vya Kamati za Bunge, siku ya tarehe 12 Machi 2019, Wabunge watapokea Wasilisho la Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Kanuni ya 97 ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016.

KUFANYA ZIARA ZA UKAGUZI WA MIRADI
Kamati zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi ya Maendeleo iliyotengewa fedha katika Bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016. Kamati zitakagua miradi ya uwekezaji liyotekelezwa na Serikali kupitia Mashirika ya Umma.  Aidha, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi mingine iliyotekelezwa na Serikali ili kulinganisha matokeo ya utekelezaji na thamani halisi ya fedha za Umma zilizotumika katika miradi hiyo.

KUFANYA UCHAMBUZI WA BAJETI
Katika vikao hivyo pia Kamati zitafanya uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti za Wizara inazozisimamia kwa Mwaka wa Fedha unaoishia 2018/2019 kwa ajili ya kufanya ulinganisho kuhusu makadirio ya matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.

KUFANYA UCHAMBUZI WA TAARIFA ZA UWEKEZAJI
Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itafanya uchambuzi wa Taarifa za Uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016.

UCHAMBUZI WA SHERIA NDOGO
Kamati ya Sheria Ndogo itafanya uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Nne Bunge kwa mujibu wa Kifungu cha 11 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016

Ratiba zote za Shughuli za Kamati za Bunge ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo Kamati hizo zitafanya ziara zinapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz. mara baada ya Kamati hizo kuanza kazi.

Imetolewa na:     Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa.

Ofisi ya Bunge
DODOMA
05 Machi, 2019
Share To:

msumbanews

Post A Comment: