Wizara ya Maliasili na Utalii imesema imeanza kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto zinazokikabili Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka ili kiendeleze hadhi yake ya kuwa Chuo cha Kimataifa.

Hatua hiyo inakuja kufuatia kupungua kwa idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaojiunga na Chuo hicho kila mwaka na kukifanya kianze kupoteza hadhi yake ya kuwa chuo cha Kimataifa.

Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii baada ya kufanya ziara katika Chuo hicho mkoani Kilimanjaro. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa moja ya shabaha ya Wizara ni kuona chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kinaendelea kuwa na hadhi ya Kimataifa.

Kuhusu hatua zilizochukuliwa amesema ni pamoja na Wizara kuendelea kufanya mazungumzo na vyombo vya udhibiti na Usimamizi wa Elimu hapa nchini ( TCU na NACTE) viangalie namna ya kuondoa masharti magumu yanayosababisha baadhi ya masomo ya wanafunzi wa kigeni yasitambuliwe chuoni hapo.

Mhe.Kanyasu ameieleza kamati hiyo kuwa sababu nyingine ya idadi ya Wanafunzi wa kigeni kupungua ni baadhi nchi kama Malawi na Kenya kuanzisha vyuo tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Shabani Shekilindi amesema Chuo hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za uhaba wa wahadhiri pamoja na uchakavu wa miundombinu.

Amesema yeye kama Mwenyekiti kupitia Kamati yake ataziwasilisha changamoto zilizopo ili ziweze kutatuliwa. Amekishauri chuo hicho kiendelee kuzitangaza kozi zinazotolewa ndani na nje ya nchi.

Naye mmoja wa Wajumbe wa kamati hiyo Mhe. Boniphace Getere amekishauri chuo hicho kiingie mkataba na watu binafsi kwa ajili kujenga mabweni yatayokayosaidia kutatua changamoto ya wanafunzi 228 kati ya 600 wanaolazimika kupanga nyumba nje ya Chuo cha Mweka.

Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilianzishwa mwaka 1963 kikiwa na wanafunzi 25 kutoka Kenya, Uganda Malawi , Cameroun na Tanzania.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: