Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, ametembekea na kukagua maendeleo ya shughuli za utekelezaji wa mradi wa maji wa vijiji vitano, mradi unaotekelezwa na Serikali, ndani ya halmashauri ya Arusha kwa ufadhili wa Idara Maendeleo ya nchini Uingereza- DFID kupitia shirika la kimataifa la WaterAid.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya,  amefanikiwa kutatua changamoto, inayowakabili wakandarasi hao, inayotokana ucheleweshwaji wa kupata kibali cha msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani ( VAT) katika ununuazi wa vifaa vya ujenzi wa miundo mbinu, kwa kuwaunganisha na kampuni ambayo, wakandarasi hao watapatiwa vifaa na kuendelea na kazi, huku akiwaahidi kufuatilia suala hilo kwa haraka na wakandarasi hao kupatiwa msamaha huo wa kodi kulingana na sheria.
Aidha amewataka wakandarasi hao sasa, kuongeza kasi ya kufanya kazi zao  na kukamilisha kwa wakati kama mkataba unavyoelekeza, ili wananchi na walengwa wa mradi huo waweze kupata maji na kuondokana na mateso wanayoyapata ya kutafuta maji kwa umbali mrefu.
Hata hivyo, Muro ameawataka wakandarasi hao, kutokana na msamaha huo wa kodi kujipanga, kutekeleza kipengele cha kuchangia maendeleo kwenye jamii katika eneo la mradi, ikiwa ni pamoja na miradi ya elimu na afya, na kuahidi kusimamia kipengele hicho cha  Corporate Social Responsibility (CSR) na kuhakikisha kitekelezwa.
" Niwatake wakandarasi wote wa mradi huu, kuhakikisha mnatekekeza kipengele cha CSR, kwa kuchangia shughuli za maendeleo ya jamii, kwenye eneo la mradi, tuna shule na vituo vya afya, jipangeni kufanya hivyo na nitasimamia hilo" amesema mkuu huyo wa Wilaya
Mkuu huyo wa wilaya amejionea shughuli mbalimbali zilizofanywa na wakandarasi wa mradi huo mkubwa,  kazi zinazohusisha ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji, matanki ya kusukumia maji, nyumba ya kutibia na kuchujia maji, nyumba za kusukumia maji, nyumba za kuhifadhia pumpu, ujenzi wa chanzo cha maji Emurtoto,  usambazaji wa mabomba ya maji na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji ndani ya vijiji hivyo vitano.
Naye Mratibu wa mradi wa shirika la WaterAid mkoa wa Arusha, Upendo Muntambo, licha ya kumshukuru na kumpongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kutembelea eneo la mradi, amesema kuwa upatikanaji wa haraka wa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani,  utaongeza  kasi ya ujenzi wa mradi huo na kuweza kumalizika kwa wakakati na kuthibitisha kuwa ziara hiyo ni afya kwa shirika na chachu ya maendeleo ya mradi huo na kumuomba kupita mara kwa mara.
"Kwa niaba ya shirika ninakushuru sana kwa kutembelea eneo la mradi nakujionea kinachoendelea, kwetu sisi ziara yako ni afya kwa mradi,nikushukuru kwa kushughulika suala la VAT, ambalo limekuwa ni kikwazo na limechelewesha mradi kwa kiasi fulani,  nikuahidi kufanyia kazi ushauri uliotoa, na nikuombe kutembelea site mara kwa mara" amesema Mratibu huyo
Hata hivyo wakandarasi hao wamemshukuru, mkuu huyo wa wilaya kwa kuwatembelea na kuanza kushughulikia suala la msamaha wa kodi (VAT), jambo ambalo limekuwa ni  kikwazo kikubwa katika utelelezaji wa mradi huo, hasa katika ununuzi wa vifaa, na kuahidi kufanya kazi kwa nguvu kubwa ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni ya Advance Company Ltd& Meero Contractors Ltd, Mhandisi Barongo Agustine, amethibitisha kuwa,  suala la kupata kibali cha msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani, limekuwa ni changamoto kubwa kwao, kiasi cha kukwamisha baadhi ya shughuli kuanza kutekelezeka kwa wakati, lakini kutokana na utatuzi huo uliofanywa na mkuu wa wilaya, tunaamini kazi itaenda kwa kasi na kuhakikisha wananchi wanaoata maji kama malengo ya serikali ya awamu ya tano.
Mradi huo unatekelezwa kwa kugawa kazi katika sehemu kubwa tatu, ambazo kandarasi hizo zimetolewa kwa makampuni matatu, ikiwa ni pamoja na kampuni ya STS Construction Company Ltd, kampuni ya Advance Company Ltd na Meero Contractors Ltd na  kampuni ya ASES Ltd.
Awali, utekelezaji wa mradi wa maji wa vijiji vitano ulianza rasmi Mei, 2017 na unategemea kukamilika mwezi Aprili, 2019 na kuhudumia watu zaidi ya elfu 10 wa vijiji vya Olkokola na Lengijave pamoja na vutongoji vitatu vya Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni ndani ya Mamlaka ya Mji mdogo Ngaramtoni.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: