Monday, 11 March 2019

DC KATAMBI AFANYA ZIARA KWENYE SHULE MBILI ZA MSINGI NA SEKONDARI AMBAZO ZIMEEZULIWA PAA ZAKE

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amefanya ziara kwenye shule mbili za Msingi na moja ya Sekondari ambazo ziliezuliwa paa zake kufuatia mvua kubwa iliyonyeesha hivi karibuni Wilayani humo.

DC Katambi amefanya ziara hiyo katika shule za msingi  Nzuguni na Ihumwa  na Sekondari ya Ihumwa ambapo aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na maafisa elimu msingi na Sekondari na kutoa maagizo kwa mhandisi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha madarasa yaliyokumbwa na dhahama hiyo yanafanyiwa matengenezo haraka ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao kama kawaida.

"Nimesikitishwa na hii kadhia mliyoipata na ndio maana nikafika hapa ili niweze kujionea mwenyewe, Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imedhamiria kutoa elimu bure hivyo changamoto kama hizi zinazojitokeza lazima tuzitatue kwa haraka, hivyo nitoe maagizo kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kupitia kwa Mhandisi kuhakikisha majengo yaliyoharibiwa yanafanyiwa ukarabati upesi ili vijana wetu waweze kuendelea na masomo yao" amesema DC Katambi.

DC Katambi pia aliwataka waalimu wa shule hizo kuhakikisha wanadhibiti utoro pamoja na tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike na kuagiza kutoa ripoti ofisini kwake kwa mtu yeyote ambaye atabainika kumpa mimba mwanafunzi.

"Ndugu zangu jukumu la kuzuia mimba mashuleni ni letu sote, wote tuwe walinzi wa hawa vijana wetu, kama tutawalea vizuri basi hapa ndipo tutakapowatengeza wakuu wa Wilaya , Mikoa na Mawaziri wa baadaye," amesema DC Katambi.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Dodoma, Joseph Mabeyo amemshukuru DC Katambi kwa kutembelea shule hizo pamoja na kutoa maelekezo kwa Mhandisi ili aweze kufanyia matengenezo madarasa yaliyoharibika na kumuomba aendelee kutolea macho sekta ya elimu kwani ndipo yalipo mafanikio ya nchi zote zilizoendelea duniani.

Mimi nakushukuru sana Mhe DC kwa kuacha shughuli zako ofisini na kufika kutuona, tumefarijika sana na hakika hii inatufanya tuone Serikali yetu chini ya Rais Magufuli inafanya kazi kwa wananchi wake, tunashukuru kwa maelekezo yako ambayo  umeyatoa," amesema Mabeyo.

*Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Dodoma.*

No comments:

Post a Comment