*Asema lengo ni kuondoa manung’uniko kwa watumishi wa taaluma moja

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Hospitali ya Aga Khan uandae skeli ya mishahara inayofanana kwa watumishi wenye taaluma zinazofafana ili kuondoa manung’uniko baina ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Ameyasema hayo kutokana na malalamiko ya watumishi wa taasisi hiyo ambao wanadai kuwepo kwa tofauti ya mishahara kwa watumishi licha ya kuwa na taaluma moja na kufanyakazi kwenye kituo kimoja.

Hayo yalisemwa jana (Jumamosi, Machi 9, 2019) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

Waziri Mkuu alisema suala la maslahi kwa watumishi ni muhimu na linatiliwa mkazo na serikali hivyo uongozi wa Hospitali ya Aga Khan fanyeni mapitio ya mishahara hasa kwa watu walio katika taaluma zinazofanana.

“Serikali imeunda Tume ya Mishahara na Motisha inayofanya mapitio ya ngazi za mishahara ili kuondoa utofauti wa mishahara kwa watumishi waliosoma ngazi moja, wenye taaluma moja wanaofanyakazi kwenye kituo kimoja.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa suala la uwiano wa mishahara kwa watumishi wenye taaluma zinazofanana ni muhimu na linapaswa lifanywe kwa watumishi wote bila ya kujali kama mtumishi huyo ni Mtanzania au anatoka nje ya Tanzania. 

Awali, Waziri Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma katika jengo hilo ikiwemo maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya wazazi. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu sh. bilioni 192, kati yake sh. bilioni 134 ni mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 10, 2019.
Share To:

Post A Comment: