Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ametoa
wiki moja kwa mtaalamu Elekezi wa Kampuni ya Archquants Service
Limited kuhakikisha inawasilisha michoro ya kazi za nje ya Chuo cha
ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Namtumbo kilichopo Mkoani Ruvuma ili
ujenzi wa chuo hicho uweze kukamilika.

Mheshimiwa Ole Nasha ametoa agizo hilo wakati wa kukagua maendeleo
ya ujenzi wa chuo hicho ambapo amesema ucheleweshwaji wa michoro
hiyo unapelekea kuchelewesha ukamilishaji wa mradi huo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ameitaka Mamlaka ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kuhakikisha wanaanzisha kozi ya
ufundi wa zana za kilimo (Agro mechanics) katika Chuo cha Ufundi na
Mafunzo ya Ufundi Stadi kilichopo Songea ili kupata vijana wengi
watakaosomea fani hiyo.

Naibu Waziri amesema ukanda wa Nyanda za Juu Kusini unategemea
sana kilimo, hivyo kuanzishwa kwa kozi hiyo kutasaidia wananchi wengi
kupata uelewa wa kina kile wanachokisoma na baadae kutekeleza kwa
vitendo.

“Serikali inatilia mkazo Elimu ya ufundi na imejielekeza katika kuhakikisha
inapanua fursa ya vijana wengi kupata Elimu ya ufundi na ndio maana
Serikali ya awamu ya Tano imeamua kuweka Vyuo vya VETA katika kila
Wilaya na Mkoa,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri Ole Nasha yuko mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku
mbili kwa ajili ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara ya
Elimu, Sayasni na Teknolojia.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA.
01/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: