Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amewataka viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji nchini kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba hawaondoki katika maeneo yao kwenda kufanya kazi za ndani wakati wakisubiri matokeo ya kuhitimu darasa la saba.

Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Manyara wakati akizungumza na viongozi hao kuhusu hali ya Elimu mkoani humo ambapo amewataka kusimamia kwa ukaribu suala hilo ili kutokatisha ndoto za watoto hao na kwamba wale wanaofanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Hakikisheni watoto wanaposubiri matokeo hawasafirishwi kwani wanapofika huko wanarubuniwa na waajiri hivyo hata matokeo yakitoka na kuonesha kuwa wamefaulu hawarejei kuendelea na masomo “ alisisitiza Naibu waziri Ole Nasha.

Kiongozi huyo ameendelea kuwasisitiza wazazi kuwa fursa za Elimu katika nchi yetu ni kubwa, ikizingatiwa kuwa Elimu msingi ni bure hivyo hakuna kisingizio tena kuwa mtoto hawezi kusoma.

“Wazazi msiwe sehemu ya kuchangia watoto wenu kwenda mjini kwa kuwa tu wanawatumia fedha kwa ajili ya matumizi bali hakikisheni mnawasimamia vyema watoto hao katika kipindi chote cha kusubiri matokeo na kuwapeleka shule pindi matokeo yanapotoka na kuonekana wamefaulu,” alisisitiza Naibu waziri Ole Nasha
Share To:

msumbanews

Post A Comment: