• WAZIRI NDALICHAKO AENDELEA KUSISITIZA KUWA ELIMU MSINGI NI MIAKA 7

Zaidi ya kiasi cha shilingi Milioni 40 zimechangwa na wadau wa Elimu  na wananchi mbalimbali wa Wilaya ya Pangani  kwa ajili ya kuchangia  ujenzi wa mabweni ya wasichana wa kidato Cha tano na sita katika shule Sekondari Mwera mkoani Tanga.

Fedha hizo zimekusanywa mara baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kuongoza harambee hiyo wakati wa kongamano la wadau wa Elimu lililoandaliwa na mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso.

Kupitia kongamano hilo la Elimu Waziri Ndalichako ameendelea kuwasisitiza wananchi kuwa muda wa elimu ya Msingi ni miaka 7 na kuwa sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho, hivyo hata kama wanafunzi wanaosoma mtaala mpya hivi sasa watasoma kwa miaka saba na kuwa suala hilo ni  la kisheria.

“Pamoja na kuwepo mtaala mpya bado elimu msingi ni miaka 7 na kuwa suala hilo lipi kisheria hivyo kama kutakuwa  na mabadiliko yoyote Serikali itashirikisha  wadau katika kutoa maoni na mwisho wa siku wadau watapata taarifa kamili, hata hivyo   serikali mkakati wake hivi  sasa ni wa kuhakikisha ina boresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia,”alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amezitaka  kamati za shule kuhakikisha zinasimamia taaluma pamoja na kuhoji kuhusu matokeo ya elimu ambayo hayaridhishi lakini pia ushirikiano wa pamoja lazima uwepo ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri kwenye taaluma Wilayani humo.

“ Mtumieni Mheshimiwa mbunge Juma Aweso awe ni mfano wenu wa kuiga, amekuwa akijitolea mfano kuwa mama yake alikuwa mama ntilie, lakini amezingatia sana elimu na hiyo ndiyo imemkomboa ndiyo maana leo hii ameweza  kuwa mbunge wa jimbo la Pangani na pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, yote hii ni kwa sababu amesusa, amesisitiza Ndalichako.

Akizungumza na wananchi katika kongamano hilo la Elimu Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah ni kuwa familia  nyingi Wilayani humo zina maisha magumu hivyo ni vyema Wilaya hiyo ikawa na  michepuo ya kidato Cha tano na sita ili wanafunzi wanaoofaulu wabaki hapo hapo kuendelea na masomo badala ya wazazi kuanza kuingia gharama za kuwapeleka kwenye shule za mbali.

“ Mheshimiwa Waziri Wilaya yetu ina shule
Moja tu yenye kidato Cha tano na sita, sasa tumejiwekea malengo angalau tuwe na shule 3 tofauti  ili wanafunzi waendelee kusoma hapa hapa pia tunahitaji Chuo Cha Ufundi kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wetu waweze kujiajiri,”alisisitiza  Mkuu huyo wa Wilaya.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Majina Umwagiliaji Juma Aweso amesema Wilaya hiyoilichelewa sana kuwekeza kwenye Elimu na hivyo amewataka wanapangani kubadilika na kuwa elimu pekee ndiyo Mkombozi wao.

“Kupitia Elimu, mtoto wa mama ntilie anaweza kuwa Mkemia, Profesa, Mhandisi, Daktari bingwa, kiongozi , hivyo elimu pekee ndiyo silaha ya kuifanya Jamii yoyote iweze kuwa na Maendeleo,”alisema Aweso.

Imetolewa na;
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
13/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: