Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu amewataka washauri elekezi ( consultant) kuhakikisha wanatimiza wajibu  katika kutekeleza majukumu yao pindi wanapokabidhiwa miradi ya kusimamia, na kuwa haipendezi miradi inapoenda kukaguliwa kuwa na masuala ya kutumbuliwa.

Dkt. Semakafu amesema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya Force Akaunti ambao ni utaratibu unaotumika kwenye ujenzi au ukarabati kwa kutumia malighafi za ujenzi na mafundi waliopo eneo husika.

Dkt. Semakafu amesema Force Akaunti ikitumika vizuri inaonyesha thamani ya Fedha lakini pia utaratibu huo hauna mabadiliko ya gharama wakati wa kutekeleza ujenzi au ukarabati tofauti na kutumia mkandarasi katika kutekeleza miradi ya Serikali.

“Force Akaunti ipo kisheria na kinachohitajika ni uzalendo, pia fedha inayotengwa kwa ajili ya ujenzi haiguswi na kuwa  hii inatakiwa ioneshe thamani ya Fedha kwa maana matokeo makubwa kwa fedha kidogo,” alisisitiza Dkt. Semakafu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Noel Mbonde  amezitaka Mamlaka za Ufundi Stadi  VETA kuhakikisha zinaleta mabadiliko ili nchi iweze kufikia malengo ya uchumi wa viwanda.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanaratibiwa na mradi wa kukuza Maarifa, Stadi na ujuzi (ESPJ) yanahusisha Wakurugenzi wa halmashauri za Kasulu,Ngorongoro,Kongwa,Nyasa, Wakurugenzi wa  Kanda VETA, Wakurugenzi wasaidizi kutoka Makao Makuu VETA, Maafisa kutoka VETA,

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
1/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: