Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka wadau wa Elimu kuhakikisha wanatumia takwimu sahihi zilizotolewa na Mamlaka husika wakati wa kuandaa machapisho yao ili kuepuka kupotosha umma.

Waziri Ndalichako amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu unaoshirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi kuwa kipaumbele cha Serikali ya awamu ya Tano ni Elimu na ndio maana Wizara hiyo imekuwa ikitengewa bajeti ya kutosha na bajeti ya Wizara hiyo haijawahi kushuka.

Waziri Ndalichako amesema kumekuwa na upotoshwaji wa takwimu zinazotolewa kwenye machapisho mbalimbali kuwa bajeti ya Wizara ya Elimu imeshuka hadi kufikia asimilia 56 suala ambalo Waziri Ndalichako amelikanusha na kueleza kuwa bajeti ya Wizara hiyo haijawahi kushuka na mpaka Juni 2018 bajeti ya Wizara hiyo ni asilimia 86.5.

“Bajeti ya Wizara ya Elimu haijawahi kushuka kwa kuwa kipaumbele cha serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ni Elimu, hivyo takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye machapisho mbalimbali sio sahihi na badala yake takwimu sahihi za bajeti ya Wizara ya Elimu ni asilimia 86.5 hadi kufikia Juni 2018,” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amewaambia wadau wa Mkutano huo wa AJESR unaofanyika Jijini Dodoma kuwa Elimu ndio nyenzo muhimu inayotoa dira na muongozo ili kuhakikisha Taifa linakuwa na watu walioelimika kwa maendeleo ya Taifa katika kufikia uchumi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Waziri Ndalichako amewataka washiriki wa mkutano huo kujadili kwa kina mafanikio, changamoto na kuwa na mikakati ya pamoja itakayosaidia Serikali kufikia malengo waliojiwekea katika Sekta ya Elimu.

Mkutano huo wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu umekuwa ukishirikisha wadau mbambali wa ndani nan je ya nchi ulianza mwaka 2008 na umekuwa ukifanyika kila mwaka.

Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Upatikanaji wa Elimu bora kufikia Tanzania ya Viwanda” umeanza leo  na utakamilika Septemba 28, 2018.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJI
25/9/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: