Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameagiza kufukuzwa kazi afisa ardhi wa wilaya ya Monduli bwana Kitundu Mkumbo kwa kukiuka sheria na taratibu za utoaji wa hati miliki za kimila.

Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo mbele ya wakazi wa kijiji cha Engarooji wilayani Monduli mkoani Arusha ambao wamekua katika mgogoro wa ardhi kwa muda mrefu hali iliyowalazimu kugawanyika katika makundi mawili yasiyoelewana, Waziri Lukuvi amefafanua kuwa mwenye mamlaka ya kumilikisha mtu ardhi zaidi ya hekari 50 ni Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee.

“Afisa huyu wa ardhi ambaye japo hapo awali mlishawahi kumsimamisha kazi kwa makosa mengune kama haya, lakini  kwa sasa makosa haya ni makubwa sana na sasa afukuzwe kazi, haiwezekani amilikishe hekari zaidi ya 1,500 kinyume na sheria” Alisema Mhe. Lukuvi.
 
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amezifuta hati zote za kimila zilizotolewa na afisa ardhi huyo kwasababu zimetolewa kinyume na utaratibu kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 ambayo hairuhusu kutoa hatimiliki za kimila zaidi ya hekari 50 bila idhini ya Rais.

Miongoni mwa watu waliomilikishwa maeneo makubwa kubwa katika kijiji cha Engarooji wilayani Monduli ni Paulo Ndari mwenye hekari 716, Lekashu Ng’ene mwenye hekari 301 na Salimu Orkoskos mwenye hekari 268 ambazo zote pamoja na nyingine Waziri Lukuvi amezifuta.
Share To:

Anonymous

Post A Comment: