Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi mdogo wa Ubunge na udiwani utakaofanyika katika jimbo la Liwale na kwenye kata 37 leo jijini Dodoma.
 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Athumani Kihamia akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi mdogo wa Ubunge na udiwani utakaofanyika katika jimbo la Liwale na kwenye kata 37.
 Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria wakati wa mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Oktoba 13 mwaka huu.
 Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa Mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo, jijini Dodoma
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi washiriki wa Mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo, jijini Dodoma leo.

Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Oktoba 13 mwaka huu katika jimbo la Liwale na kwenye Kata 37 za Tanzania Bara wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na Kanuni za uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mbarouk Salim Mbarouk ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kutoka katika maeneo yenye uchaguzi.
Jaji Mbarouk amewataka Wasimamizi hao kufanya kazi kwa ufanisi, uhuru, uwazi na bila kuegemea upande wowote ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.
Amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.

“ Tunakutana hapa ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi, natumaini mtatumia fursa hii kubadilishana uzoefu katika kutekeleza jukumu hili lililo mbele yenu”  Amesema Jaji Mbarouk.

Jaji Mbarouk ametoa wito Wasimamizi hao waepuke madhara yanayotokana na ukiukaji wa Sheria, Kanuni na taratibu za Uchaguzi akisisitiza kwamba katika kipindi hiki chaguzi  zinafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya Kisiasa, kutoaminiana na wakati mwingine kutawaliwa na mihemko ambayo imekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Aidha, amewaeleza Wasimamizi hao kuwa wameaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo kwa kuwa wanao uwezo mkubwa wa kufanya kazi hivyo wajiamini na kujitambua.
Ametoa wito kwa Wasimamizi hao kuhakikisha kwamba wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi na wanawatumia vyema wasaidizi walio nao katika maeneo yao ya kazi kwa matokeo bora.
“Naomba mjue mna jukumu la kuimarisha imani ya wananchi pamoja na wadau wote wa uchaguzi kwa Tume. Hivyo mfanye kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, bila kuegemea upande wowote.Kufanya kazi kwa uhuru na kwa uwazi kutasaidia kudumisha amani katika maeneo yenu ya Uchaguzi” Amesema.
Kuhusu kufanyika kwa Uchaguzi huo mdogo Oktoba 13 mwaka huu,  Jaji Mbarouk amesema kuwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 kikisomwa pamoja na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura 292, ni jukumu la Tume kusimamia, kuendesha na kuratibu uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi.
Amesema kwa nyakati tofauti Tume imepokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Ubunge katika jimbo la Liwale.

Pia amefafanua kuwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali ya Mitaa, Sura, 292 alitoa taarifa ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 37 kutoka katika Halmashauri 27 zilizopo katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara.
Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti wa NEC  Jaji Mbarouk Salim Mbarouk ameeleza kuwa jumla ya wagombea 6 waliteuliwa kugombea ubunge katika jimbo la liwale ambapo mgombea mmoja alijitoa baada ya uteuzi huo kukamilika.
Ameongeza kuwa katika Kata 37 za Tanzania Bara jumla ya wagombea 56 waliteuliwa kugombea udiwani katika Kata hizo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: