Thursday, 27 September 2018

Viongozi wa Kijiji wafunga ofisi na kutimka, kisa operesheni ya Bangi


Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wananchi wa kijiji cha Kisimiri Juu kilichopo tarafa ya King’ori wilayani Arumeru walikiacha kijiji chao kwa muda huku viongozi wao wakifunga ofisi zao na kukimbia kisa operesheni ya bangi iliyofanywa na vikosi vya Jeshi la Polisi Alfajiri leo hii.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alisema walipata taarifa kwamba kuna kiasi kikubwa cha bangi kinatarajia kusafirishwa siku ya leo ndipo walipoandaa askari hao ambao walifanikiwa kufika eneo la tukio na kupata jumla ya magunia 27 yenye uzito wa Kilogramu 25 kila gunia shambani kwa mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa pamoja na Misokoto 583 ya Bangi.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba kwa sasa Jeshi la Polisi mkoani hapa linawatafuta viongozi wa kijiji cha Kisimiri Juu kwa kukiuka agizo la Serikali linalomtaka kila kiongozi katika eneo lake ahakikishe kwamba hailimwi bangi.

“Tunaendelea kuwatafuta viongozi wa kijiji pamoja na kamati zake za ulinzi na usalama na mkondo wa sheria utachukua nafasi kwani wao kama viongozi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha katika eneo lao hakuna biashara yoyote ya Madawa ya kulevya inayofanyika”. Alifafanua Kamanda Ng’anzi.


Kamanda Ng’anzi alisema kwamba Jeshi hilo mkoani hapa lipo makini na litaendelea na mapambano dhidi ya dawa ya kulevya katika maeneo mbalimbali na kubainisha kwamba katika eneo la mpaka wa Namanga matukio ya uingizaji wa madawa umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni  wa Jeshi hilo mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP) Elias Mwita alisema kwamba  operesheni hiyo sio ya kwanza kufanyika katika eneo hilo na itakuwa endelevu kuhakikisha kwamba zao hilo haliendelei kulimwa.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: