Askari wa Usalama Barabarani wilayani Korogwe mkoani Tanga, ambaye jina lake halijafahamika, anatuhumiwa kumpiga dereva wa basi la Tahmeed Coach baada ya kumkamata kwa mwendokasi.

Kamishna Msaidizi wa Polisi, Leonce Rwegasira akizungumza kwa niaba ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, alisema wanaendelea kulifanyia uchunguzi tukio hilo.

“Ni kweli tukio lipo. Tunaendelea na uchunguzi utakaotuelekeza ni hatua gani za kuchukua dhidi ya mtuhumiwa kama tutabaini kosa.”

Taarifa za kupigwa kwa dereva wa basi hilo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Ijumaa iliyopita baada ya video zilizokuwa zikionyesha tukio la wafanyakazi wa basi hilo pamoja na abiria, wakimshambulia kwa maneno askari huyo.

Video hiyo pia ilionyesha abiria na wafanyakazi wa basi hilo ambalo lilikuwa likitokea Nairobi, Kenya kuelekea Dar es Salaam wakimlalamikia askari huyo kwa kumpiga dereva wa basi hilo.


Video hiyo inaonyesha jinsi mabishano hayo yalivyokuwa yakiendelea huku mfanyakazi mmoja wa basi na abiria wakilalamika kuwa kitendo kilichofanywa na askari huyo si cha kiungwana.

“Kama anakosa si ungemtoza faini baada ya kumuonyesha uthibitisho, kwa nini mnampiga?” anaonekana mfanyakazi wa basi hilo akimhoji mmoja wa askari aliyekuwa akiwataka wanyamaze.

Sauti nyingine inasikika ikisema, “Trafiki anampiga dereva, kamwandikia faini lakini bado anaendelea kumpiga dereva kutoka Dar kuelekea Nairobi, kwa kosa la kuzidisha spidi. Je, hii ni haki.”

Sauti nyingine ambazo zinazosikika katika video hiyo ni pamoja na “una-power (nguvu) gani ya kumpiga dereva… aah mwache ampige, mwache ampige…. endelea kumpiga.”

Askari mmoja katika video hiyo anaonekana akihoji ushahidi wa dereva huyo kupigwa na hapo sauti nyingine inasikika, “Amempiga...mimi ninao ushahidi. Nimemuona akimpiga, mimi ninao ushahidi.”

Dereva huyo alipotakiwa kueleza ukweli wa tukio hilo, licha ya kuthibitisha kutokea, hakutaka kuingia kwa undani akisema alikuwa barabarani akiendesha gari.

“Nikweli tukio limetokea lakini kwasasa siwezi kuzungumza niko barabarani ninaendesha gari nikifika Dar es Salaam nitakupigia kueleza ukweli wa tukio” alisema.

Alipotafutwa baada ya kufika dereva huyo alisema hawezi kuzungumza mpaka apewe maelekezo na bosi wake juu ya kipi azungumze.

Baadaye, Mwananchi lilimtafuta msimamizi wa mabasi hayo upande wa Dar es Salaam katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT), Nguzo Abdallah ambaye alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa Ijumaa iliyopita huko Korogwe.

Alisema dereva huyo aliyemtaja kwa jina mojo la Salehe, alisimamishwa na askari akimtuhumu kuendesha gari kwa mwendokasi.

“Ukweli ni kwamba, baada ya askari kumsimamisha dereva, alimweleza amezidisha mwendo wa kilomita 57 kwa saa kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani ambayo inamtaka kwenda kilomita 50 kwa saa katika eneo hilo,” alidai Abdallah.

Alisema baada ya kukamatwa, dereva alimtaka askari huyo amtajie eneo kilipo kibao kinachoonyesha 50, lakini askari hakumtajia na badala yake alimwambia ajiongeze la sivyo atapelekwa mahakamani.

Alisema dereva aliendelea kugoma akimwambia kuwa anamuonea kauli iliyosababisha askari huyo kuanza kumshambulia kwa matusi na kipigo.

“Baada ya kuona tukio hilo, abiria walishuka na kuanza kumsaidia dereva asipigwe na askari huyo na wengine wakawa wanarekodi tukio hilo kwa simu zao,” alisema meneja huyo.

Mbali ya Abdallah, meneja wa kampuni ya mabasi hayo, Hassan Singano alisema taarifa za tukio hilo zinashughulikiwa na dereva wao alifika kituo cha usalama barabarani Korogwe kuhojiwa.

“Taarifa nilizonazo hadi sasa, ni kuwa dereva wetu alikuwa akiendesha gari nje ya kilomita ambazo zipo kwenye kibao, askari walimkamata, lakini dereva akadai aonyeshwe hizo picha zinazomuonyesha ameendesha kwa kasi na kibao kinachomtaka atembee kilomita 50 kwa saa, lakini hakuonyeshwa.

“Katika kubishana pale, ikafikia hatua askari kumshambulia kwa matusi na kipigo, lakini suala hilo bado linafuatiliwa na kampuni. Kama kutakuwa na taarifa zozote tutakujulisha,” alisema Singano.

Na Jackline Masinde, Mwananchi
Share To:

Anonymous

Post A Comment: