Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Richard Mayongela (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na viwanja vya ndege kuchangia uingiaji wa watalii nchini. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax Mabula. 

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imejipanga, kupitia kaulimbiu yake, kuifungua Tanzania kwa ulimwengu kupitia sekta ya utalii nchini, kwa kuimarisha usafiri wa anga ili kuhakikisha watalii wote wanafikia vivutio vyote vya utalii kwa haraka zaidi.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela,  alipokuwa akizumgumza na waandishi wa habari Siku ya Ushiriki wa Mamlaka katika Tamasha la Urithi Wetu litakaloanza Jumatatu Oktoba Mosi, 2018 kwa Mkoa wa Dar es Salaam.


“Viwanja vyetu vya ndege ndiyo milango mikuu wa watalii, hivyo tupo hapa kuwaambia wananchi, wadau pamoja na jumuiya za kimataifa kwamba sasa kuna fursa ya kutangaza vivutio vya kitalii kupitia viwanja vyetu vya ndege kwa kuwa vinatumika kwa usafiri wa anga lakini pia tunaweza kuvitumia kibiashara kwa kutangaza vivutio vyetu,” alisema Mayongela.


Mayongela pia ametoa wito kwa watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza vivutio vilivyopo kupitia viwanja vya ndege lakini pia kuwaeleza wadau kwa njia mbalimbali zilizopo Tanzania ili watalii wanapowasili waweze kupata picha halisi ya maeneo ya kutembelea wakiwa nchini.


Aidha  ameongeza kwamba mamlaka hiyo ina mtandao mkubwa na inasimamia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali, ambavyo vipo kila sehemu penye vivutio vya utalii na wamejiimarisha kuhakikisha huduma bora ya usafiri wa anga.

“Sehemu ya kaskazini mwa nchi yetu ambako ndiko kuna vivutio vingi, vipo viwanja vya ndege vya kutosha, tuna kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), kiwanja cha Lake Manyara ambacho kimejengwa kwa mkakati wa kutumika kwa watalii na kinafanya vizuri sana kwa kuingiza watalii wengi, vilevile tuna mpango wa kujenga kiwanja kipya katika Mkoa wa Manyara,” alibainisha.


Akizungumzia miundombinu ya viwanja vya ndege kwa Kanda ya Kusini, ameeleza kwamba serikali imefanya maboresho ya kiwanja cha Mtwara kwa lengo moja kuu la kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo maeneo hayo.


“Serikali inaboresha kwa kufanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa kiwanja cha ndege cha Mtwara, pamoja na sababu za kiuchumi lakini pia lengo ni kuvutia watalii wengi zaidi ili waweze kushuhudia vivutio vilivyopo, si hivyo tu,  lakini pia Kilwa Masoko tuna kiwanja, Lindi tuna kiwanja, Nachingwea mpaka Masasi kote tuna viwanja, ” Alisema.


Akizungumzia upande wa Nyanda za Juu Kusini, amebainisha kwamba baada ya ukarabati mkubwa kukamilika,  kutakuwa na kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe, Njombe, na Iringa kutakuwa na viwanja vizuri vya ndege ili kuhakikisha kwamba vivutio vilivyopo Tanzania vinafikika kwa urahisi.

Katika hatua nyingine,  Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof Audax Mabula,  ameeleza kwamba Tamasha la Urithi Wetu lililobuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii lina madhumuni makuu mawili likiwemo la kuwezesha kuonyesha fursa zote zinazoizunguka tasnia hii.


“Madhumuni makuu ni kuendeleza, kutambua na kuhifadhi urithi wetu wa utamaduni kwa ajili ya kizazi kilichopo na kinachokuja lakini pili ni kubadili urithi wetu wa utamaduni kuwa zao la utalii,  hayo ndiyo malengo makuu mawili,” alisema Prof. Mabula.


TAA wametoa msaada wa fulana 100 kwa ajili ya washiriki wa tamasha la Urithi Wetu, ambalo litafikia tamati Oktoba 6, 2018 kwa kufungwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Imeandaliwa na Idara ya Uhusiano Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Share To:

msumbanews

Post A Comment: