Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge unatarajiwa kuanza siku ya Jumanne tarehe 4 Septemba, 2018 na kumalizika tarehe 14 Septemba, 2018 Jijini Dodoma. Shughuli zitakazofanyika katika Mkutano huu ni kama ifuatavyo:-

1.0 KIAPO CHA UAMINIFU
Kutakuwa na Kiapo cha Uaminifu kwa Mhe. Eng. Christopher Kajoro Chizza Mbunge wa Jimbo la Buyungu aliyechaguliwa kwenye Uchaguzi Mdogo tarehe 12 Agosti, 2018.

2.0  MASWALI
Katika Mkutano huu wa Kumi na Mbili, wastani wa maswali 125 ya Kawaida yanatarajiwa kuulizwa na Wabunge. Aidha, wastani wa Maswali 16 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yanatarajiwa kuulizwa kwa siku ya Alhamisi tarehe 6 na 13 Septemba, 2018.

3.0 MISWADA YA SERIKALI
Bunge pia linatarajia kupitisha kwa hatua zilizobaki Miswada mitano (5) ya Sheria ambayo ilisomwa Mara ya Kwanza katika Mkutano wa Kumi na Moja (11) wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 91. Miswada hiyo ni :-
  1.  Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018 [The Dodoma Capital City (Declaration) Bill, 2018];
  2.  Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018 [The Teacher’s Professional Board Bill, 2018];
  3.  Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2018 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.2) Bill, 2018];
  4.  Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2018 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.3) Bill, 2018] na
  5.   Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018 [The Public Private Partnership (Amendment) Bill, 2018].

4.0 TAARIFA ZA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE
Kamati ya Sheria Ndogo itawasilisha taarifa zake Bungeni zinazohusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.

Ratiba yote ya Mkutano wa Bunge inapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz.

Imetolewa na:-       Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano,
Ofisi ya Bunge,
DODOMA.
3 Septemba, 2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: