Picha haihusiani na habari hapa chini.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Kisumba, Kalambo mkoani Rukwa, Lusekelo Mwakyesa (47), amefariki dunia akiwa darasani wakati akisimamia mtihani wa darasa la saba.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:30 alasiri katika Shule ya Msingi Mkapa iliyoko katika kijiji cha Kateka, kata ya Matai wilayani Kalambo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema Septemba 3 majira ya asubuhi, mwalimu huyo alikwenda katika kituo chake cha kazi na kuomba ruhusa kwa Mwalimu Mkuu, Athuman Rashid, kuwa anahisi anaumwa malaria, hivyo anataka kwenda kununua dawa.

Alisema siku iliyofuata, mwalimu mkuu huyo alimuuliza mwalimu huyo kama ataweza kwenda kusimamia mitihani ya darasa la saba katika kituo alichopangiwa na kusema anaweza.

Aidha, alisema siku hiyo mwalimu huyo alifika katika eneo ambalo wasimamizi wote walielekezwa kufika ili wapewe maelekezo na waliulizwa kama kuna msimamizi ambaye ana matatizo ya kiafya na hakuna aliyejitokeza, hivyo walipelekwa katika vituo vyao.

Kamanda Kyando alisema juzi Mwakyesa alifika katika chumba cha mtihani na kuendelea kusimamia wanafunzi. Alisema asubuhi alimaliza mtihani wa kwanza na kupumzika kwa ajili ya mtihani wa mchana.

Aliporudi katika chumba cha mtihani, alisema mwalimu huyo alitoa maelekezo yote kwa wanafunzi na kugawa karatasi za mitihani na za kujibia maswali na alipomaliza alikwenda kukaa katika kiti alichoandaliwa ili apumzike huku akiendelea kuwasimamia wanafunzi hao.

“Baada ya kukaa, aliinama kama amejilaza katika meza iliyokuwa mbele yake kwa muda mrefu bila kuinua kichwa ndipo mmoja wa wanafunzi, Joel Mwajungwa, aliona maji yakitiririka kutokea miguuni kwa msimamizi huyo kitendo kilicho mshtua na kutoka nje kumwita mgambo aliyekuwa akilinda usalama katika maeneo ya shule,” alisema Kamanda Kyando.

Alisema baada ya mgambo huyo kuingia darasani na kumtingisha, msimamizi huyo hakuamka na alipoangalia yale maji alibaini kuwa ni haja ndogo na kutoa taarifa kwa msimamizi mkuu aliyefika na gari na kumpeleka katika kituo cha afya cha Matai kwa ajili ya matibabu.

Kwa mujibu wa Kamanda Kyando, walipofika kituo cha afya walipokewa na mganga wa zamu, Chapanga Chapanga na alimfanyia uchunguzi na kubaini kuwa alikwishafariki dunia.

Alisema walipokagua katika begi lake walikuta dawa aina tano ambazo ni Aluu, Panadol, Piriton, NTZ na Tsonizide na inasadikika kuwa mwalimu huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
Share To:

Anonymous

Post A Comment: