Wednesday, 12 September 2018

KATIBU WA CCM NYAMAGANA AWATAKA WATENDAJI WA KATA NA SERIKALI ZA MITAA KUTEKELEZA ILANI YA UCHAGUZI WA CCM KWA UMAHIRI NA UZALENDO


Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Nyamagana Ndg Salum A. Kalli ametoa rai hiyo hivi leo kwenye kikao chake kilichowakutanisha watendaji wa serikali 98,  ikiwa watendaji wa Kata 18, mitaa 80 pamoja na watendaji 18 wa Chama Cha Mapinduzi kata zote.

Ndg Kalli ametumia kikao hicho kuwakutanisha watendaji wa serikali na wasimamizi wa serikali ambao ni makatibu wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya kata kwa dhima ya kudumisha ushirikiano wa kikazi. Ndg Kalli amewapatia maelekezo ya kikatiba pamoja na Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 kwa kuwasa kuwa wazalendo kwa nchi yao na waaminifu kwa Chama tawala ambacho ndio waajili wao.

"Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na CCM ndio Chama kilichoweka mkataba na wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kupitia Ilani yake, na watekelezaji wakuu wa Ilani ni ninyi ambao kwa nafasi zenu ni makatibu wa CCM ndani ya dola, sitaraji mtaisema vibaya CCM au kutenda kinyume na CCM na matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM taifa  Mhe Dkt John Pombe Magufuli, ninatazamia mtekeleze majukumu yenu kwa ushirikiano wa karibu na makatibu wa CCM nje ya dola ambao ni watendaji wa Chama kwa ngazi za mitaa na Kata". Ndg Kalli amesema

Ndg Kalli amewasihi watendaji hao kuzingatia utawala bora unaoimarisha umoja na mshikamano kazini sanjali na kuzingatia taratibu za urejeshaji wa taarifa za miradi ya maendeleo, Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara  pamoja na uwasilishaji wa taarifa za fedha kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Ibara ya 145/146. Amewataka wajiekeze katika utendaji unaosikiliza na kutatua kero za wananchi na kutekeleza wajibu wao bila kushurutishwa ili kutokutoa mianya ya kukitukanisha Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi.

Naye Afisa raslimali Watu na Utawala halmashauri ya Jiji la Mwanza Ndg Sigufridi Asani Kaunara akishukuru kwa kikao hicho ambacho kimetoa mwelekeo wa falsafa ya Hapa kazi tu. Amwemwehidi watendaji wa serikali kutoa ushirikiano wa dhati  katika utelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2015-2020 ikiwa ni pamoja na kuongeza watendaji wengine ili kuleta ufanisi.

Kikao hicho kimefanyika ukumbi wa CCM Nyamagana na kuhudhuliwa na seketariet ya Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Nyamagana pamoja na Afisa raslimali watu na Utawala halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Imetolewa na
Idara ya Siasa na Uenezi
Chama Cha Mapinduzi Nyamagana
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: