DKT . KALEMANI ATOA MWEZI MMOJA KWA VIJIJI VYOTE VYA JJIJI LA ARUSHA KUPATA UMEME

Mkuu wa Mkoa Arusha, Mrisho Gambo (kushoto) akizungumza na wakazi wa Kimondolosi, wilaya ya Arusha mjini, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani (katikati) ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REAIII) wilayani humo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wakazi Kijiji cha Kimondolosi Kata Olasiti Wilaya ya Arusha mjini.
Wakazi wa Kata ya Olasiti, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliyekuwa akizungumza kuhusu kuwapatia huduma ya umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (wa Tatu kushoto) akikagua nguzo za umeme katika Kata ya Terati, zitakazotumika kuwapatia Umeme wananchi wa eneo hilo mkoani Arusha. Wa Pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Na Zuena Msuya, Arusha.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa mwezi mmoja kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa vijiji vyote vilivyopo katika Jiji la wa Arusha vinaunganishwa na huduma ya umeme. Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo jijini Arusha baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA III) katika Vijiji vilivyopo jijini humo na kujionea hali ya ukosefu wa nishati ya umeme.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, Wananchi hawafurahii kucheleweshewa kupata huduma ya umeme hali ya kuwa wengine walikwishalipia huduma hiyo.

" Haipendezi na haifurahishi machoni mtu kajitahidi kujibana na kujenga nyumba yake nzuri na ya kisasa, lakini anakosa umeme wakati uwezo wa kumuunganishia upon a vifaa vipo, sasa kwa nini asiunganishwe.?," alihoji Dkt. Kalemani. Kutokana na hali hiyo, aliwataka TANESCO kuunda vikosi kazi mbalimbali vitakavyosaidia kazi ya kusambaza umeme kwa wananchi kwa haraka.

Aidha, alimwagiza mkandarasi anayesambaza umeme jijini humo, kampuni ya Nipo Group, kuhakikisha kuwa anawafungia umeme wananchi wa Kimondorosi katika Kata ya Olasiti mkoani Arusha na kuhakikisha kuwa kila siku anatoa ripoti ya utekelezaji wa mradi kwa mtendaji wa mtaa huo hadi atakapomaliza kuweka umeme kwa wananchi . 

Alisema kuwa, mkandarasi huyo anapaswa kufanya kazi hiyo ili kuwaondolea kero ya ukosefu wa umeme wananchi hao ambao wamekaa kwa muda mrefu bila kupata huduma hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kutoa agizo hilo litakalopelekea wananchi hao kupata umeme kwani wananchi hao walishamlalamikia kuhusu kukosa huduma hiyo.

Vilevile, mmoja wa wananchi katika Kata hiyo, Clementina Mushi alimuomba Waziri wa Nishati kuhakikisha kuwa umeme huo unafika kwa wananchi wote bila kurukwa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: