Tuesday, 14 August 2018

Waziri Mwakyembe aitaka TCRA kutoa muongozo kwa wenye visimbuzi nchini


Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kufanya mazungumzo na wamiliki wa visimbuzi vya AZAM, DSTV na ZUKU ili kutoa muongozo wa nini kifanyike juu ya hatma yao ya kutoruhusiwa kuonesha channeli za umma kinyume leseni zao.

Akizungumza hayo na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Waziri Mwakyembe alisema kuwa visimbuzi vya AZAM, DSTV na ZUKU vilikiuka mkataba wao wa leseni na kuonesha chaneli za umma ikiwa ni pamoja na kuwatoza fedha watazamaji.

“TCRA watoe muongozo wa nini kifanyike kwa visimbuzi vilivyokiuka utaratibu, ikiwa sasa watapenda kuonesha channeli hizo za umma wapewe utaratibu wa nini cha kufanya” alisema Waziri Mwakyembe

Aliongeza kuwa uamuzi wa TCRA kuwataka watoe channeli hizo za umma umezingatia sheria, ambapo amevipongeza visumbuzi hivyo kwa kufuata sheria na kutoendelea kuonesha channeli hizo.Aidha, Waziri Mwakyembe alifafanua kuwa visimbuzi vinavyoruhusiwa kuonesha channeli za umma bila kuwatoza fedha watazamaji ni Startimes, Digtek na Continental, kulingana masharti ya aina ya leseni yao.

Alitaja masharti hayo kuwa ni visimbuzi hivyo vimelipa gharama ya leseni mahsusi ambayo ni dola laki nne, miundombinu ya urushaji matangazo yake iko hapa nchini ambayo ni minara na satellite, maudhui yake ni yakitanzania na gharama ya visimbuzi vyao ni nafuu.

Waziri Mwakyembe, alisema kuwa masharti ya leseni ya kurusha maudhui ama channeli za kulipia ni pamoja na gharama ndogo ya leseni ambayo ni dola laki moja, maudhui yake ni kwa ajili ya soko la kimataifa.

Aliongeza masharti mengine kuwa ni, miundombinu ya kurusha matangazo ipo nje ya nchi mfano ya DSTV iko Dubai, ZUKU nchini Kenya na AZAM ikiwa  huko nchini Mauritius, pamoja na matangazo yake kutegemea kurushwa kwa satelite.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa ufafanuzi juu ya visimbuzi visivyoonesha chaneli za ndani mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Afisa Mwandamizi Mkuu wa Sheria toka Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Dk. Philip Filikunjombe na kulia ni Afisa Mwandamizi Mkuu wa Masuala ya Utangazaji toka mamlaka hiyo Bw. Andrew Kisaka.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi juu ya visimbuzi visivyoonesha chaneli za ndani mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Afisa Mwandamizi Mkuu wa Masuala ya Utangazaji toka Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Bw. Andrew Kisaka (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) alipokutana na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es Salaam ili kutoa ufafanuzi juu ya visimbuzi visivyoonesha chaneli za ndani, kushoto ni Afisa Mwandamizi Mkuu wa Sheria toka Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) Dk. Philip Filikunjombe.Picha na –Eliphace Marwa (MAELEZO).

No comments:

Post a Comment